Harmonize apagawisha maadhimisho uhuru wa Tanganyika

Muktasari:

Kucheza na kutikisa kichwa ni kati ya mambo yaliyoendelea wakati Rajab Abdul maarufu Harmonize, msanii wa muziki  nchini Tanzania akitoa burudani katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika yanayofanyika uwanja wa CCM Kirumba leo Jumatatu Desemba 9, 2019.

Mwanza. Kucheza na kutikisa kichwa ni kati ya mambo yaliyoendelea wakati Rajab Abdul maarufu Harmonize, msanii wa muziki  nchini Tanzania akitoa burudani katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika yanayofanyika uwanja wa CCM Kirumba leo Jumatatu Desemba 9, 2019.

Baada ya kutajwa kuwa yupo uwanjani hapo na atatoa burudani, mamia ya wananchi walianza kushangilia huku wakipeperusha bendera za Taifa.

Msanii huyo anayetamba na wimbo wa Kushoto Kulia pamoja na Uno, aliimba wimbo unaoeleza mambo mbalimbali yaliyofanywa na Serikali tangu mwaka 2015 wenye maudhui ya kumsifu Rais John Magufuli na kusababisha baadhi ya kusimama na kuanza kucheza, akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wakati viongozi wakicheza na kutikisa vichwa, wananchi walishindwa kujizuia na kushuka jukwaani, kwenda katikati ya uwanja huo ili kumshuhudia vyema msanii huyo.

Baada ya Harmonize kumaliza kutoa burudani, wananchi walirejea katika majukwaa kwa ajili ya kumsikiliza Rais Magufuli.