Harmonize atakuwa msanii wa pili kuondoka Wasafi

Muktasari:

Ikitokea hivyo atakuwa amefuata nyayo za Rich Mavoko ambaye mwaka 2018 alijiengua katika kundi la Wasafi linaloundwa na Diamond Platnumz, Mbosso, Rayvanny, Queen Darlin, Lavalava na Harmonize mwenyewe

Dar es Salaam. Ukisema msanii Harmonize yupo mbioni kujiondoa katika kundi la Wasafi utakuwa hujakosea kabisa.

Na ikitokea hivyo atakuwa amefuata nyayo za Rich Mavoko ambaye mwaka 2018 alijiengua katika kundi la Wasafi linaloundwa na Diamond Platnumz, Mbosso, Rayvanny, Queen Darlin, Lavalava na Harmonize mwenyewe.

Jana Jumatano Agosti 21, 2019 meneja wa kundi la Wasafi,  Sallam amesema Harmonize haonekani katika matamasha ya Wasafi Festival yanayoendelea Mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa amevunja utaratibu wa tamasha hilo kwa kujitenga na wenzake

Amesema mbali na kuvunja utaratibu, pia ameomba kuvunja mkataba na kundi hilo.

Akizungumza katika televisheni ya Wasafi, Sallam amesema katika tamasha la Wasafi lililofanyika mjini Mwanza, Harmonize alitumia usafiri binafsi, kufanya baadhi ya mambo yaliyotoa tafsiri kuwa amejitenga.

Kwa mantiki hiyo muda wowote Harmonize anaweza kuwa nje ya kundi hilo ikiwa mkataba huo utavunjwa na kufuata nyayo za Mavoko aliyejiondoa Wasafi mwaka 2018 baada ya kupeleka malalamiko ya kutoridhishwa na mkataba wake ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Kwa sasa Mavoko yupo chini ya lebo ya Bilionea Kid na anatamba na wimbo wa Usizuge alioutoa Mei 30, 2019.

Katika maelezo yake ya jana, Sallam amesema Harmonize moyo wake haupo Wasafi lakini ukweli ni kuwa bado ana mkataba na kundi hilo.

“Kwanini nasema hivyo, Harmonize ameshatuma barua ya maombi Wasafi kuvunja mkataba wake na yupo tayari kufuata sheria zote.”

“Sisi tumependezwa na hatua yake kwa sababu labda kuna vitu ameona akivifanya atafika mbali,” amesema Sallam.

Kuhusu kujitenga na wenzake Sallam amesema, “Hili jambo si sawa kulingana na maudhui ya tamasha hilo. Maudhui ya Wasafi Festival ni umoja. Msanii akiamua kuacha kuambatana na wasanii wenzake ambao wapo pamoja katika tamasha ni kwenda kinyume.”

“Sisi katika tamasha letu hatupendi kutengeneza matabaka, tumeamua kuwa kitu kimoja, siyo kwamba Diamond, Rayvany hawakuwa na uwezo wa kutumia usafiri wao binafsi kama alivyofanya Harmonize” amesema Sallam.

Meneja huyo amewaomba radhi wasanii wote walioshiriki tamasha la Mwanza kutokana na Harmonize kufanya jambo hilo, kwamba uongozi wa Wasafi haukuwa na taarifa.

Amebainisha kuwa Harmonize amefanya jambo la kuhatarisha taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kumpandisha jukwaani msanii ambaye hakuwepo katika ratiba ya tamasha hilo.

“Alikuja na msanii kutoka nje na hatukujua kama alishamchukulia kibali au laa,  kwa hiyo unaona kabisa anafanya vitu ambavyo vinaweza kuingiza taasisi katika tatizo,” amesema.