Harmonize kujiondoa WCB, ni hatari kwa Ali Kiba?

Saturday August 24 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Ni siku chache zijazo, tutaanza kuzisikiliza nyimbo za Harmonize bila kibwagizo cha ‘Wasafi Records’ na ‘Eyo Laiza’.

Mwanamuziki huyo, ambaye jina lake halisi ni Rajab Abdul Kahali ameandika barua ya kujitoa katika lebo ya Wasafi Records.

Msanii huyo ambaye nyimbo zake za ‘Kwangalu’ na ‘Show Me’ zimeleta gumzo nchini, bila shaka ataleta upinzani mkubwa kwa wasanii wa lebo hiyo akiwamo Diamond mwenyewe.

Kwa sababu Harmonize ameishi WCB, anajua nguvu yao, anajua udhaifu wao, anajua sehemu ya kupita na kufanya vitu vya tofauti.

Hakuna ubishi kuwa mashabiki wa muziki watasubiri kwa hamu kila wimbo utakaotoka kwa Harmonize na hakuna shaka kuwa atapata mashabiki ambao hawampendi Diamond.

Licha ya watu wengi kudhani kuwa WCB itatetereka, hali haiwezi kuwa hivyo kwa sababu Diamond na wenzake wataamka na kufanya vitu vya tofauti zaidi wakijua sasa wapo katika mapambano halisi.

Advertisement

Hilo haliwezi kukwepeka kwa sasa kwamba Diamond atajipanga zaidi kwa sababu katika akili yake anajua kuwa Harmonize anakwenda kuwa mpinzani wa kweli tofauti na Ali Kiba, ambaye upinzani wake umetengenezwa zaidi na mashabiki.

Upinzani huu utakuwa halisi, kwa sababu ni ngumu wakati mwingine kutofautisha wimbo wa Diamond na Harmonize, labda sasa tofauti itakuwa ni midundo na melodi.

Ushindani huo unaweza ukampoteza kwa muda Ali Kiba, ambaye mashabiki wamekuwa wakilazimisha ili aonekane kuwa mpinzani wa Diamond.

Utajiuliza kwanini mashabiki wanalazimisha? Hoja hapa ni kuwa unamlinganishaje msanii ambaye kwa mwaka anatoa nyimbo zaidi ya 10 na mwingine ambaye anatoa wimbo mmoja.

Ni rahisi kutetea kuwa idadi haijalishi, lakini ni ukweli kuwa Diamond anafanya muziki kibiashara tofauti na Ali Kiba, ambaye kwa kiasi kikubwa anafanya kama ‘kujifurahisha zaidi’.

Bila shaka mashabiki wa Ali Kiba na wale wanaomchukia Diamond, kwa muda fulani watashangilia chochote kinachofanywa na Harmonize na kila wimbo wa msanii huyo utapendwa na kundi hilo la mashabiki bila kujali kiwango chake.

Kwa namna fulani jambo hilo linaweza kufanya ushindani wa Diamond na Harmonize kuwa mkali kwa muda fulani na hasa itategemeana na jinsi Harmonize atakavyoondoka WCB kama ni kwa shari au kwa amani.

Kwa vyovyole vile, upinzani wa Diamond na Harmonize unaweza kufunika nyota ya Ali Kiba kama akishindwa kucheza karata zake vizuri.


Advertisement