Hatima ya Kabendera kujulikana Februari 24

Muktasari:

Kesi ya uhujumu  uchumi inayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania, Erick Kabendera imekwama kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya hakimu anayeisikiliza, Janeth Mtega kupata udhuru.

Dar es Salaam . Kesi ya uhujumu  uchumi inayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania, Erick Kabendera imekwama kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya hakimu anayeisikiliza, Janeth Mtega kupata udhuru.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha Sh173 milioni.

Leo Jumatatu Februari 17, 2020 ni mara ya pili kesi hiyo kuahirishwa ndani ya wiki moja. Februari 10, 2020 kesi hiyo iliahirishwa baada ya upande wa mashtaka kuomba mahakamani hiyo ipange tarehe inayofuata yaani Februari 11, 2020.

Februari 11, 2020 upande wa mashtaka uliomba mahakama  hiyo kuahirisha ili mshtakiwa apate nafasi ya kukutana na mawakili wa Serikali kwa ajili ya kukamilisha  mchakato wa kumaliza kesi yake.

Leo wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo amepata udhuru na kuomba mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Simon ameieleza mahakama hiyo  mbele ya Hakimu mkazi, Vicky Mwaikambo  wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

"Kesi hii ilikuja kwa ajili ya kutajwa na hakimu anasikiliza kesi hii amepata udhuru, naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na shauri hili,” amedai wakili Simon.

Simon baada ya kueleza hayo Reginald Martin ambaye ni wakili wa Kabendera  aliomba mahakama  ipange tarehe fupi kwa sababu wapo katika hatua za mwisho kukamilisha makubaliano ya kumaliza kesi hiyo.

Hakimu Mwaikambo baada ya kusikiliza hoja za upande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 24, 2020.

Kabendera amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza alifikishwa Kisutu Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha Sh173.2 milioni.