Breaking News

MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Hatimaye Tanganyika, Zanzibar zaungana - 14

Tuesday April 23 2019

Viongozi waasisi wa Muungano Abeid

Viongozi waasisi wa Muungano Abeid Karume(kulia)na Mwalimu Julius Nyerere. 

By William Shao

Jana tuliona jinsi harakati za Muungano zilivyozidi kukua, huku Wamarekani wakitumiana ujumbe kuelezea kufurahishwa na hatua iliyofikiwa, lakini wakitahadharisha uwezekano wa Urusi kufanya jambo lolote bila ya kutarajia. Pia walielezana kuwa makini kuihusisha Marekani na muungano. Sasa endelea.

Wakati Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere akiwa amemuagiza spika kuitisha kikao cha dharura, Marekani ilikuwa ikifuatilia na balozi wake, William Leonhart alitoa taarifa nchini kwake kuhusu maendeleo hayo.

Alisema Nyerere “ameitisha kikao cha dharura cha Bunge kitakachokutana Jumamosi, kujadili suala la Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar”.

Mjini Unguja Aprili 24, mara baada ya kukagua gwaride la heshima, Sheikh Karume aliwahutubia wananchi wa Zanzibar akizungumzia muungano baada ya yeye na Nyerere kusaini hati.

“Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utadumu kwa muda mrefu. Sote tutafaidi na wala hautawadhulumu Wazanzibari,” alisema katika hotuba yake.

Siku iliyofuata, Rais Nyerere alilihutubia Baraza la Taifa (kwa sasa Bunge) akiliomba liukubali mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Advertisement

“Kwanza nataka kuwaombeni radhi kwa mambo mawili, matatu. Kabla ya kurudi majumbani baada ya mkutano wenu wa mwisho, mlikuwa mmekubaliana kuwa mtakutana tena tarehe 28, mwezi huu. Na makamu wa rais alikuwa amewaambia kwamba ilikuwa nia yangu kuwatangazieni mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano hapo mtakapokutana,” alisema Nyerere.

“Kwa bahati mbaya ilibidi nitumie uwezo mlionipa katika sheria yenu moja ya utaratibu wa kazi zenu. Nikaahirisha mkutano wenu kwa majuma mawili; yaani mpaka tarehe 12 mwezi ujao.

“Pia kabla ya tarehe hiyo kufika imenibidi tena kuwaita hapa. Natumaini mtakubali kwamba sababu zote mbili; ya kuahirisha mkutano wenu na ya kuwaiteni kwa haraka, ni za maana. Nimewaiteni katika kikao hiki cha haraka ili kuwaomba mthibitishe mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri yetu na Jamhuri ya Unguja.

“Parliament (Bunge) hii ndiyo Baraza Kuu la Wananchi wa Tanganyika. Hapana jambo lolote kubwa linalohusu katiba, au mikataba au sheria za nchi hii ambalo laweza kupitishwa na mtu au kundi lolote ila Baraza hili. Mambo yote ya aina hiyo hayana budi yafikishwe katika baraza hili na ni juu yenu kuyakubali au kuyakataa. Leo naleta mbele yenu mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Unguja kuzifanya ziwe nchi moja.

“Tanganyika na Unguja ni nchi za jirani kwa kila hali. Kwa umbali kila mmoja wenu anajua jinsi tulivyo karibu. Inasemekana kuwa kwa kweli kutoka Unguja au Pemba hadi Tanganyika ni karibu zaidi kuliko kutoka Unguja hadi Pemba. Kadhalika kwa historia. Wakati mmoja Unguja na mwambao wa Tanganyika vilikuwa chini ya serikali moja, yaani serikali ya Sultani wa Unguja. Ni ajali ya historia tu iliyofanya tusiendelee kuwa nchi moja.

“Wakati wakoloni wa Kizungu walipoanza kuzigawanya nchi za Afrika Mashariki walikubaliana kwamba Unguja na Pemba na mwambao wa Kenya viwe chini ya ulinzi wa Mwingereza, bali mwambao wa Tanganyika na bara yake viwe chini ya Ujerumani.

“Hivyo ndivyo tulivyoacha kuwa nchi moja. Na baada ya vita vikuu viwili vya kwanza sisi tulipowekwa chini ya Waingereza, Unguja na Tanganyika tuliendelea kuwa nchi mbili tofauti kwa sababu ya utaratibu wa kutawaliwa na Mwingereza.

“Jambo moja ambalo uhuru wetu unatupa katika Afrika ni nafasi ya kuona kama wale tuliokuwa kitu kimoja bali tukatengwa na mkoloni hatuwezi tukaungana tena kuwa kitu kimoja, madhali sasa tumemwondoa mkoloni? Tanganyika na Unguja ni nchi ndugu. Tunashirikiana ujirani kwa historia, lugha, mila, tabia na siasa. Udugu wa Afro-Shiraz Party na Tanu wote mnafahamu.

“Udugu baina ya viongozi wa vyama vyote viwili haukuanza jana. Basi tunazo sababu zote hizo za kutufanya tuungane, tuwe kitu kimoja. Juu ya yote hayo kuna shauku ya umoja wa bara la Afrika. Basi, mimi badala yenu, na President Karume badala ya ndugu zetu wa Unguja na Pemba tulikutana Unguja siku ya tarehe 22 mwezi huu tukatia sahihi mkataba wa umoja kati ya nchi zetu mbili.”

Nyerere alieleza umuhimu wa umoja huo na umuhimu wake kwa Afrika.

“Tukifanikiwa, wale wasiopenda umoja wa Afrika watastuka. Watashtuka kwa sababu watatambua kwamba kweli umoja wa Afrika unawezekana. Kwa hiyo watafanya kila jitihada kutufanya tushindwe. Ni wajibu wetu kujihadhari. Ni wajibu wetu kuulinda umoja huu,” alisema.

“Tumwombe Mwenyezi Mungu atusaidie sisi na ndugu zetu wa Unguja na Pemba kutimiza wajibu huu.”

Bunge lilikubali kupiga muhuri ombi hilo, na serikali hizo zikaungana siku iliyofuata, yaani Aprili 26, 1964.

Suala hilo lilimfanya balozi wa Marekani nchini Kenya, William Attwood alitume taarifa kuelezea kilichojiri.

“(Mwandishi wa Nyerere, Dunstan) Omar ametuambia kulingana na taarifa za vyombo vya habari zilizoenea mjini Dar es Salaam leo, kwamba nguvu kubwa ya utawala katika mambo ya serikali zote mbili (usalama, fedha, mambo ya nchi za nje, huduma za umma) zitakuwa mikononi mwa Serikali ya Muungano, lakini Zanzibar itaendelea kushughulikia mambo ya serikali yake yenyewe,” alisema katika ujumbe wake.

“Sheria za Tanganyika ndizo zitakazokuwa na nguvu ya mamlaka kote (Tanganyika na Zanzibar). Alilifikiria hili kuwa muhimu sana kwa sababu, kwa kuwa sheria ya kuwaweka watu kizuizini ingeweza kutumiwa kuwakamata watu wenye siasa kali Zanzibar.”

Ndipo Jumapili ya April 26, 1964, likatimia lile ambalo Mwalimu Nyerere alilitafuta kwa kipindi chote cha siku 100; Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Baada ya sherehe fupi za kihistoria, ndipo Sheikh Abeid Aman Karume alipokaririwa na gazeti The Nationalist and Freedom, kutoka Ikulu, akisema kuwa “Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar utatufaidisha sisi sote. Hautakuwa kikwazo kwa watu wa Zanzibar.”

Itaendelea kesho

Advertisement