Hazina Saccos kujenga kitega uchumi cha Sh52 bilioni

Sunday October 13 2019

 

By Benny Mwaipaja, WFM [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Saccos) kimeazimia kujenga kitega uchumi cha kisasa kwa gharama ya  Sh52 bilioni kupitia mradi wa Njedengwa uliopo Jijini Dodoma.

Mradi huo unalenga kukuza uchumi wa Mkoa wa Dodoma na Taifa kupitia kodi.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Oktoba 13, 2019 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi wa chama hicho, Aliko Mwaiteleke  wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina.

Amesema mradi huo upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.

Mwaiteleke amesema mpaka sasa upembuzi yakinifu wa mradi huo utakaojengwa kwa njia ya ubia kati ya Hazina Saccos na mwekezaji kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 22  kupitia utaratibu wa Jenga, Endesha na Hamisha (Build, Operate and Transfer - BOT), mwekezaji atagharamia ujenzi wote na kuendesha kwa muda ambao utakubaliwa ndani ya mkataba.

Amesema mradi huo unasimamiwa na Kamati ya watu saba wakiongozwa na Profesa Esta Eshengoma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wajumbe wake kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),  Bodi ya Manunuzi ya Umma (PSPTB), Kituo Cha Uwekezaji (TIC) na Chuo Kikuu cha Ardhi ambao kwa sasa wanafanya kazi ya kusaka mwekezaji ili kufanikisha mradi huo.

Advertisement

Akifafanua juu ya mradi wa Njedengwa, Mwaiteleke amesema upo mbioni kuanza  na unategemewa kuwa chachu ya maendeleo ya chama hicho kwa kukiingizia kipato kutokana na shughuli zitakazokuwa zikifanyika kupitia.

 Amesema mradi huo pia utahusisha ujenzi wa hoteli ya kisasa, kumbi za  mikutano, majengo ya ofisi,  viwanja vya michezo na bwawa maalumu la kuogelea.

Hazina Saccos yenye wanachama 5,600 ina mtaji wenye thamani ya Sh10 bilioni zikiwa ni fedha taslimu na mali wanazozimiliki ikiwamo ardhi, zimekuwa na manufaa makubwa kwa wanachama.

“Mwaka jana pekee kupitia akiba na mikopo,  tulipata faida ya Sh64 milioni  na kila mwanachama alipewa gawio la asilimia 20 kulingana na hisa zake,” amesema Mwaiteleke.

Naye Meneja wa Hazina Saccos, Festo Mwaipaja amesema chama hicho hakiko kwa ajili ya wafanyakazi wa Wizara ya Fedha pekee, bali watumishi wote wa Serikali wanaruhusiwa kujiunga na chama hicho isipokua vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni Jeshi, Polisi na Usalama wa  Taifa.

Akifungua Mkutano Mkuu huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga ameipongeza Hazina Saccos kwa kuwapatia viwanja wanachama wake na kuwataka walivipata waviendeleze haraka ili kuondokana na changamoto ya malazi kwa kuwa baadhi walipata viwanja hivyo tangu mwaka jana.

Aidha, ameipata kongole Hazina Saccos kwa hatua waliyofikia ya kutafuta mwekezaji katika mradi wa Njedengwa ambao utaongeza mapato ya Ushirika na kuwataka viongozi na wanachama kuhakikisha wanazingatia taratibu Sheria na Kanuni ili kufanikisha mradi huo muhimu.

Advertisement