Helikopta ya JWTZ yatua Serengeti kuchukua mwili wa mtoto wa Mabeyo

Muktasari:

Mwili wa Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo unasafirishwa kutoka Serengeti na kupelekwa jijini Dar es Salaam. Nelson akiwa na mwenzake wamefikwa na mauti leo asubuhi Jumatatu

Serengeti. Helikopta ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imewasili uwanja wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania kwa ajili ya kuuchukua mwili wa Nelson Mabeyo.

Nelson ambaye alikuwa rubani wa ndege ya Kampuni ya Auric air yenye namba 5H-AAM amepata ajali katika uwanja huo akiwa na Nelson Orutu ambaye ni rubani mwanafunzi na wote kwa pamoja wamefariki dunia papo hapo.

Miili ya wawili hao akiwamo wa rubani huyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ilihifadhiwa katika Zahanati ya Soronera ikisubiri taratibu zingine.

Helikopta hiyo imetua saa 8.35 ikiwa na watu wanne.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdini Babu  amesema helikopta hiyo imeelekezwa ichukue mwili mmoja wa mtoto huyo wa Mabeyo na mwili wa Orutu aliyekuwa naye utabaki kusubiri ndege nyingine itakayokwenda Serengeti ikiwa na wataalamu wa masuala ya anga kwa ajili ya uchunguzi wa ajali hiyo.

Kiongozi wa msafara kutoka JWTZ, Meja Makimboka amesema wataalam wa jeshi watafika wakati wowote kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

"Pamoja na wataalam wa anga jeshi pia linaleta wataalam wake kwa ajili ya uchunguzi, sisi tunachukua mwili tu kwa sasa," amesema.

 

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi