Henga: Watumishi LHRC tunatishiwa

Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga (Kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alipotembelea ofisi ya kituo Dodoma

Muktasari:

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema watendaji wa kituo hicho wanapewa vitisho kutokana na kazi wanazofanya.

 

Dodoma. Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema watendaji wa kituo hicho wanapewa vitisho kutokana na kazi wanazofanya.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 27, 2020 mbele ya wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakiongozwa na mwenyekiti wa tume hiyo,  Jaji mstaafu  Mathew  Mwaimu walipotembelea ofisi za LHRC mjini  Dodoma.

Henga amesema pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na LHRC, watumishi wake wanapokea vitisho kutokana na kazi za utetezi wanazofanya, “hatukati tamaa katika kuwasaidia Watanzania.”

Kwa mujibu wa Henga, wamekuwa wakipishana na Serikali kwa maelezo wao ni wapinzani, lakini kinachowaponza ni  kutafuta demokrasia kwa wananchi.

"Hata rangi tunayotumia wanaifananisha na chama fulani cha upinzani, sisi hatufungamani na upande wowote kinachotuponza ni kutetea demokrasi tu," amesema Henga.

Ameeleza jinsi wanavyonyimwa taarifa na haki ya kufuatilia baadhi ya mambo ikiwemo ombi la kufuatilia uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019.

Jaji Mwaimu ameeleza umuhimu wa kituo hicho kufanya kazi pamoja na tume yake bila kuchoka lakini akasisitiza haki iendane na wajibu.

Jaji Mwaimu amesema kazi inayofanywa na LHRC inapaswa kuungwa mkono na wapenda haki kote ingawa kuna baadhi ya maeneo,  ikiwemo serikalini kuna baadhi ya watu hawajui haki za binadamu.