MAKALA YA MALOTO: Hili ni kosa kukuza sakata la kina Kinana

Thursday February 20 2020

 

By Luqman Maloto

Katika siasa ya vyama, mambo ambayo hupunguza uungwaji mkono wa kiongozi ndani ya chama chake ni kuonekana hakubaliki na viongozi wengine. Na kwenye propaganda moja ya silaha zinazoweza kutumika kupunguza uungwaji mkono wake ni kuvumisha kuwa haelewani na wenzake.

Hoja ndani ya aya mbili zilizotangulia si sifa kwa chama kuvumisha habari kuwa viongozi fulani ama wastaafu au walio ngazi za chini, hawamkubali au wanasigana na kiongozi mkuu aliye madarakani.

Sasa, katika propaganda ni mtaji mkubwa kwa wasiomtakia mema kiongozi aliye madarakani, wanapopata taarifa kuwa haivi na viongozi wengine. Huvumisha na kuchochea utambi ili kukuza mgogoro na hata kufanikisha mpasuko.

Pia, katika propaganda, kwa wenye kumtakia mema kiongozi huyo wanapopata taarifa kuwa ni kweli haelewani na viongozi wengine, kwao huwa ni pambano la kuhakikisha ukweli unageuzwa au habari hazivuji ili kutibu mpasuko.

Haijawahi kuwa sifa kwa chama cha siasa kutangaza kiongozi wake anapigwa vita au anahujumiwa na ama viongozi wengine au wanachama wa kawaida.

Hiyo ndiyo hoja nyuma ya sakata la makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kutuhumiwa kuwa na mkakati wa chini kwa chini kutaka kumhujumu Rais John Magufuli. Taarifa hii haikupaswa kutangazwa na kupewa uenezi mkubwa.

Advertisement

Sababu ni Kinana na Makamba ni viongozi. Utumishi wao wa muda mrefu ndani ya chama na Serikali umewajengea heshima na ufuasi mkubwa.

Wanaheshimika na wanaaminika miongoni mwa wana CCM wengi na Watanzania kwa mamilioni.

Wana-CCM wanafahamu kuwa kabla ya Rais Magufuli, chama chao kilihudumiwa na Makamba kisha Kinana kwa nyakati tofauti. Wapo wengi hawakupendezwa na uongozi wao na kuna wengine walikoshwa.

Wachukue wale waliokoshwa na uongozi wao, sasa watafsiri ndani ya habari kwamba hawamuungi mkono Rais Magufuli, na wanakula njama ya kuhakikisha hafanikiwi katika uongozi wake au wanajipanga kumkwamisha asiwe Rais kwa muhula wa pili.

Je, huoni kama wenye kuwaheshimu na kuwapenda Kinana na Makamba, utakuwa unawapa ujumbe na wao waanze kutomuunga mkono Rais Magufuli?

Na kadiri maneno yanavyokuzwa ndivyo ujumbe unavyopaa. Matokeo yake kundi la wenye kuwaunga mkono kina Kinana linaongezeka. Wapo ambao pengine hawakuwa wakimuunga mkono Rais Magufuli, ila walinyamaza kwa kuhisi wapo peke yao. Taarifa ya Kinana na Makamba inawachangamsha na kuwapa tafsiri kuwa wapo wengi.

Na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe. Ana ufuasi wake. Watu wanamheshimu. Kutangaza kuwa hamuungi mkono Rais Magufuli ni kuwafanya watu wanaoamini katika Membe kuanza kutomuunga mkono Rais Magufuli.

Kwa kutambua hilo katika propanga, hoja za kwamba Kinana, Makamba na Membe wanamhujumu Rais, zingepaswa kushughulikiwa chini kwa chini ili kulinda hadhi ya Rais ambaye pia ni Mwenyekiti CCM.

Uzuri inafahamika kuwa chanzo cha tuhuma ni watu wanaojiita eti ni watetezi wa Rais Magufuli.

Ingepaswa hao watetezi waitwe wahojiwe na mamlaka za chama, kwa sababu nao ni wana-CCM. waeleze ni wapi walikozitoa habari husika na ushahidi walio nao. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alipozisikia habari za Membe kutajwa, haraka alimwita akajieleze kwake kuhusu tuhuma hizo.

Ulikuwa uamuzi wa kushangaza, mtu anatuhumiwa lakini ndiye anaitwa badala ya kuanza na mtoa tuhuma ili aeleze ushahidi aliokuwa nao. Ndipo Membe angeitwa akajibu.

Uvujishaji wa sauti za viongozi hao, wakimteta Rais Magufuli nalo lilikuwa jambo la hovyo. Lilikuwa tangazo kuwa Rais Magufuli hakubaliki ndani ya chama chake, kiasi cha viongozi wengine waandamizi na wastaafu kumsengenya kila uchwao. Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM, kutaka Kinana, Makamba na Membe waitwe kwenye kamati ya maadili haukuwa mbaya. Tatizo ni kuutangaza kwenye vyombo vya habari.

Advertisement