Hoja ya Sugu matokeo urais Tanzania kupingwa mahakamani yawaibua wanasheria

Muktasari:

  • Wanasheria Tanzania wamesema kuna haja ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria nchini humo ili kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Dar es Salaam. Siku moja kupita baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema),Joseph Mbilinyi maarufu Sugu kutaka sheria za uchaguzi zibadilishwe ili matokeo ya urais nchini Tanzania yapingwe mahakamani kama ilivyo kwa ubunge, wanasheria wameibuka na kuunga mkono suala hilo.

Sugu alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana Ijumaa Aprili 3,2020 wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2020/21 ambapo alisema uwapo wa tume huru ya uchaguzi utafanya uchaguzi uwe huru na haki na matokeo ya Rais yapingwe kortini.

Kwa sasa, matokeo ya Rais yakishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yanabaki kama yalivyo na hakuna sheria inayoruhusu matokeo hayo kupingwa mahakamani.

Leo Jumamosi Aprili 4, 2020 Mwananchi limezungumza na wanasheria mbalimbali kuhusu hoja hiyo ya Sugu ambapo  wamekuwa na maoni tofautitofauti.

Wakili Dk Onesmo Kyauke amesema suala la kupinga matokeo mahakamani ni zuri kwani linafanyika na kuna nchi nyingi Afrika zinafanya hivyo ikiwamo Malawi na Kenya.

Amesema kuna umuhimu wa kuwa na kipengele cha kwenda mahakamani kwa sababu  mtu anaweza akawa hajashinda hana hata asilimia 20 lakini akadai kuwa ameibiwa na kwa sababu hakuna chombo kilichopewa mamlaka ya kuangalia kuwa madai yake ni ya kweli ama siyo kweli inaweza kusababisha machafuko.

“Lakini kwa muda huu ambao tunao kwa muda wa uchaguzi ni ngumu kufanya haya mabadiliko madogo hivyo nafikiri tungeenda tu kwenye uchaguzi kwa katiba tuliyonayo baada ya hapo tukajaribu kukaa chini na kuendeleza wazo la kuwa na katiba mpya,” amesema Kyauke

“Inatakiwa kuwe na sheria kuwa  matokeo yakipingwa itakuwaje, nani atashtakiwa, utaratibu wa kisheria utakuwaje kwa maana nyingine rais akishashinda hata suala la kuapishwa litachukua muda kama mwezi mmoja, itakuwaje kama matokeo yakitenguliwa, tutarudi kwenye uchaguzi vipi, ni sababu gani za kufanya matokeo yatenguliwe kwa hiyo ni mchakato mrefu,” amesema

Kyauke anaungwa mkono na wakili Jebra Kambole anayesema hoja ya Sugu ina mashiko akisema kuzuia kupinga matokeo ya Rais inaminya haki ya msingi ya wananchi kusikilizwa na kushiriki kwenye namna ya uongozi wa nchi ambayo ipo kwenye ibara ya 21 ya katiba ya nchi.

Kambole amesema Ibara ya 13 kifungu kidogo ca sita ya katiba ya Tanzania inasema kama kuna mtu hajaridhika na jambo lolote ana haki ya kuvifikia vyombo vya uamuzi.

“Kwa hiyo unapokuwa unazuia hivyo ina maana unazuia watu wasivifikie vyombo vya uamuzi pale wanapokuwa wana manung’uniko moyoni mwao kwa namna ambavyo uchaguzi umeendeshwa kwa hiyo haki ya kuvifikia vyombo vya uamuzi vinakiukwa,” amesema Kambole

Amesema watu wana haki ya msingi ya kusikilizwa na vyombo ambavyo ni huru ambayo ni mahakama ambayo licha ya changamoto ndogondogo watu wanaiamini.

“Katiba yetu inakataza kupinga matokeo ya Rais mahakamani, mtu wa upande mmoja akishachaguliwa basi wa upande mwingine hana ruhusa ya kwenda kupinga.”

“Tunashangaa kwa nini akishachaguliwa huna ruhusa ya kwenda kupinga, kwa sababu tuna shangaa kwa nini matokeo ya ubunge yanapingwa ya diwani yanapingwa kwa nini ya Rais hii tunakiuka haki za binadamu za kusikilizwa,” amesema

Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) nchini Tanzania, Onesmo Ole Ngurumwa amesema hiyo ni hoja nzuri ila kinachotakiwa ni katiba mpya.

“Ni hoja nzuri na ndiyo maana tunataka katiba mpya kimsingi katiba mpya ambayo tuliyokuwa tumetengeneza ilisharuhusu kabisa kupinga matokeo ya raisi mahakamani,” amesema