Hospitali nyingi za rufaa nchini hazina hadhi:CAG

Muktasari:

  • Ripoti hiyo iligundua kuwa hospitali zinakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu kama vile vitanda na maabara.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebainisha kuwa hospitali za rufaa zinakabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa na zinafanya kazi kuliko uwezo wake.

Ripoti hiyo baada ya kuwasilishwa bungeni, baadaye ilisomwa hadharani na CAG, Profesa Mussa Assad, ilibainisha hospitali nyingi zilipandishwa hadhi kuwa za rufaa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kiutawala lakini si kazi halisi.

Pia, ilibainisha kuwa hospitali tano za rufaa zilizotembelewa na wakaguzi, zinafanya kazi kama vituo vya chini vya kutolea huduma kwa sababu tangu zilipopandishwa hadhi, miundombinu yake haijawahi kuboreshwa kulingana na idadi ya watu wanaoongezeka.

Ripoti hiyo iligundua kuwa hospitali zinakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu kama vile vitanda na maabara.

“Zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa waliohudhuria hospitali hizo wangeweza kutibiwa kwenye hospitali za mwanzo,” ilibainisha ripoti ya CAG.

Ukaguzi wa CAG unaonyesha kuwa wagonjwa wanatumia muda mrefu kusubiri huduma kwenye hospitali hizo kutokana na wingi wagonjwa ambao hata hivyo hawapati huduma wanazostahili kutoka hospitali ya rufaa.

“Kati ya watu saba, wanne miongoni mwao hawakupata dawa na huduma kama vile upasuaji huku hali mbaya zaidi ikibainika kwenye hospitali ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula ambayo haikuweza kutoa huduma nyingine nne kati ya tano za rufaa ambazo zinatakiwa kutolewa.”

Ropiti imebainisha kuwa asilimia 80 kati ya 100 ya huduma za afya za msingi zinazohitajika katika hospitali hizo za rufaa zinapatikana katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Tanga.

Hali hiyo ilikuwa tofauti na zilizoko pembezoni kama Ligula ya Mtwara, Kitete ya Tabora na Mpanda iliyopo mkoani Katavi.

“Upungufu mkubwa zaidi wa idadi ya wataalamu ulibainishwa katika hospitali za Mkoa wa Mpanda, Kitete na Ligula, ambazo ziko katika sehemu mbalimbali za nchi.

CAG amependekeza Wizara ya Afya ianzishe utaratibu wa kudhibiti mtiririko wa wagonjwa ili kwanza waboreshe huduma zinazotolewa katika hospitali za rufaa.

Mapendekezo hayo yametokana na wagonjwa kumiminika kwa wingi kwenye hospitali hizo za rufaa wakiamini zinatoa huduma bora za afya kuliko hospitali za msingi.