MIAKA 20 BILA NYERERE: Hotuba ya Mwalimu Nyerere, Kuzungumza uzanzibari si fahari

Tuliijenga nchi mpya. Imara. Ni imara tu, na uimara wake ulikuwa unasifiwasifiwa sana. Lakini imetikiswa. Na nyufa tumeziona. Imetikiswa na nyufa tumeziona. Nyingine katika paa, nyingine katika dari, nyingine kutani na nyingine katika misingi.

Tunachotaka ni kwamba mtikisiko usiendelee. Tuchomee. Tuichomee iwe imara zaidi. Kwa hiyo matumaini ni kwamba tunaona hivyo wote tunaona hivyo, nchi yetu imetikiswa. Nitaeleza zile nyufa mimi ninazoziona. Nitazieleza baadaye.

Tunachotaka ni kwamba nyufa hizo zieleweke na tukubaliane kwamba kazi yetu ni kuziziba. Na tupate uongozi unaoelewa hivyo, kwamba kazi ni kuziba nyufa tulizoziona katika taifa letu. Kazi si kuendelea kulitikisa taifa. Litabomoka. Halitabaki. Sasa nyufa gani hizo. Ya kwanza mliniambia Muungano Mwalimu. Ufa wa kwanza ni Muungano. Wote mnajua. Mnaniambia ‘Mwalimu Muungano sasa ni imara zaidi kuliko miaka ishirini iliyopita?’

Ilipotikisika ufa mmoja mkubwa tuliouona ni katika Muungano. Watu wazima wameuzungumza Muungano, kama tuuvunje au uendelee. Ilikuweko hatari ya kuvunjika kwa Muungano, wala haijesha.

Watu wamezungumza Uzanzibari. Baadhi ni viongozi wetu. Wanajivunia Uzanzibari. Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga. Wapo, si wengi, lakini wapo.

Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi. Ivunjike. Tusiwe na nchi moja tuwe na nchi mbili. Ni jambo linazungumzwa. Tunataka kiongozi na viongozi watakaoelewa hivyo.

Huu, kuzungumza Uzanzibari si fahari. Si jambo la fahari. Hatima yake mtavunja nchi. Zanzibari. Mtu mwenye akili hawezi kufikiri Mzanzibari hana akili. Hawezi akautukuza Uzanzibari kwa kujiita sisi Wazanzibari na wao Watanganyika. Sisi Wazanzibari na wao Watanganyika.

Nadhani ile ina usalama ndani yake. Kwamba Uzanzibari ule na Utanganyika ule una usalama ndani yake. Hatima yake Zanzibar itajitenga.

Zanzibar ikijitenga kutokana na ulevi tu, ‘sisi Wazanzibari wao Watanganyika’, ulevi tu, ulevi hasa ulevi wa madaraka. Ikitokea hivyo kwamba ‘sisi Wazanzibari na wao Watanganyika’, wakumbuke kwamba Muungano ndio unaowafanya wanasema sisi Wazanzibari wao Watanganyika.

Nje ya Muungano hawawezi kusema hivyo. Nje ya Muungano hakuna Wazanzibari. Nje ya Muungano kuna wao Wapemba sisi Waunguja (vifijo). Nataka mjue hivyo. Nataka mjue hivyo. Nje ya Muungano hakuna sisi Wazanzibari wao Watanganyika. Hakuna.

Kinachowafanya sasa wajiite sisi ni ubaguzi wa kuwabagua Watanganyika. Wakiishakuwabagua Watanganyika, ile dhambi ya ubaguzi haifi, inaendelea. Dhambi ya ubaguzi ukishakuitenda inaendelea ni sawasawa na kula nyama ya mtu. Ukila nyama ya mtu utaendelea tu kuila.

Mtamaliza, mtatengana na Watanganyika halafu mara mtakuta kumbe sisi si Wazanzibari. Kuna Wapemba kuna Waunguja. Mtakuta hivyo.

Wapemba watapata msukosuko kidogo aah ooh! Mtakuta kumbe kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtakaa salama. Hamwezi kukaa salama baada ya kutenda dhambi ya kubagua watu wa nchi yenu ile ile moja. Mkawaita wale wao na hawa sisi.

Dhambi ile haiishii hapo. Ndivyo historia ilivyo. Ni sheria ya historia si sheria ya Mwalimu Nyerere. Huwezi kufanya ubaguzi wa namna hiyo halafu dhambi ile ikuache hapo hapo, hapana. Itakuandama.

Namalizia hilo hapo. Ninalolisema kwa Wazanzibari nalisema kwa Watanganyika. Zanzibar wanaweza wakajitenga. Wanaweza wakajitenga hivi kwa ujinga, kwa ulevi, kwa ujinga hata kwa ujinga wa viongozi wao wanaweza kujitenga. Wanaweza wakajitenga hivi.

Na Watanganyika wakabaki wameduwaa tu. ‘Loh Wazanzibari hawa wamefanyaje. Wanatuacha wenzetu hawa wanatuacha jamani. Wanakwenda zao wenzetu’.

Wakawaacha Watanganyika wameduwaa. Watanganyika walioachwa wameduwaa kwa kitendo cha Wazanzibari kuwakimbia watabaki wamoja. Hawataparaganyika. Narudia. Wazanzibari wanaweza wakatoka. Wakajitenga wenyewe tu. ‘Sasa wengine wana bendera sisi hatuna bendera kwa nini wengine wana wimbo wa taifa sisi hatuna, kwa nini,’ basi … si wote wanaosema hivyo, ni viongozi wanaosema hivyo. Basi, halafu wakajitenga. Wakawaacha Watanganyika wameduwaa.

Wakiwaacha Watanganyika walio katika hali hiyo, Watanganyika wanaowashangaa Wazanzibari katika kuwaacha, Watanganyika hao watakuwa salama. Watakuwa salama. Watanganyika wakiwakataa Wazanzibari, kwa tendo la dhambi ile ile, ‘sisi Watanganyika, wao Wazanzibari’. Wakautukuza usisi Tanganyika. Na kwa hiyo wakawafukuza Wazanzibari. Hawabaki salama. Hapatakuwa na Tanganyika.

Wakishakujitenga tu Wazanzibari wale. Wakishakujitenga tu Wazanzibari. Wako kando hivi. Mmewafukuza. Mmejidai wakubwa nyinyi … mkawatimua. Mkapata Yeltsin wenu hapa akawatimua. Hambaki.

Kwani mtasema je. Mtakuwa mmeshasema sababu ya kuwafanya wale wao na ninyi ni ninyi, wao vipi… Halafu mbaki ninyi. Maana wako watakaosema Wazanzibari tu, Wazanzibari kana kwamba kuna kabila lao Wazanzibari. Mmewabagua.

Mtaanza nyumba za Wapemba mtaziingilia pale sasa hivi. Viko vijumba vijumba vya Wapemba huku. Waliwahi kukimbia baadhi yao walikimbia wakati uleee zamani.

Vijumba vya kwanza vitapitia ‘Wapemba, Wapemba’. Mtamaliza vya Wapemba. Halafu mtakuta ninyi mliokuwa mnajiita sisi Watanganyika mtakapoanza kuchoma nyumba za Wapemba mnazichoma moto zile, mtakuta ah! Si sisi.

Sisi hawa wote si wamoja. Mbona za Wapemba tunachoma za Wachaga hatuchomi kwa nini. Maana Wachaga si wazawa bwana. Hapa kuna wazawa sasa unachoma za Wachaga tu?

Mtakuta hakuna watu wanaitwa Watanganyika. Mtakuta mlijidanganya tu mnadhani kuna watu wanaitwa Watanganyika. Hakuna. Kuna Wagogo kuna Wanyamwezi kuna Wasukuma kuna Wazanaki kuna Wakurya kuna Wamwera …eh! Wengi sana. Siwezi kuwataja wote.

Mtakuta hakuna kitu kizima hivi kinaitwa sisi Watanganyika. Na madhali mmefanya dhambi ya kusema wao Wazanzibari si wenzetu dhambi ile ile itawatafuna ninyi.

Na mimi nasema Mwenyezi Mungu anisamehe, mnastahili iwatafune. Hamwezi kutenda dhambi kubwa namna ile bila adhabu. Na adhabu zingine zimo mle mle ndani ya kitendo. Hazisubiri.

Hilo la kwanza. Kwa hiyo, la kwanza ninalosema tunao ufa wa Muungano. Ufa wa kwanza kabisa mkubwa kabisa …Tunataka Rais Mtanzania.

Rais tunayemtaka ni Mtanzania. Hatuwezi kupata Rais Mtanzania asitoke ama Zanzibar ama Tanganyika. Atatoka ama Zanzibar ama Watanganyika.

Lakini hatumchagui kwa sababu ya Uzanzibari wake. Hatumchagui kwa sababu ya Utanganyika wake. Na akiuweka mbele Uzanzibari wake akauweka mbele Utanganyika wake, tunajua huyu hatufai.

Hiyo ndiyo sifa mama. Kwa sababu tunayemtaka ni Rais wa Tanzania. Mimi niko hapa kuzungumza habari ya Rais wa Tanzania. Mimi nilikuwa wa kwanza, tunaye wa pili, na sasa namsemea wa tatu. Tunataka Rais wa Tanzania. Hiyo ndiyo sifa yake ya kwanza. Ndiyo sifa mama. Hana hiyo hatumtaki hata angekuwa na sifa nyingine zote. Atavuja nchi yetu. Hatufai. Ya kwanza.

Ya pili inafanana kidogo na hiyo. Inafanana kidogo na hiyo. Rais wa nchi yetu anachaguliwa kutokana na Katiba ya Tanzania. Na akiishakuchaguliwa anaapishwa.

Kama ni Mkristu, kwa Biblia. Kama ni Mwislamu kwa Kuruani. Hatuchagui mtu asiyemwamini Mungu. Lakini tukimchagua tutatafuta utaratibu wa kumwapisha. Ataapa. Hata asiyekuwa muumini tutamwapisha kwamba atailinda na kuitetea Katiba ya Tanzania. Asipoilinda tunamjua ni msaliti. Tutamwapisha. Ataapa. Lazima kabisa. Hata kama si muumini. Na kwa mujibu wa Katiba yetu si lazima mtu awe mwamini Mungu kuwa Rais. Hata kidogo.

Lakini tutamwapisha. Umechaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu. Unaapa kuilinda. Ataapa kwa huyo Mungu wake au akili yake anayoijua lakini atatuapia. Ataapa kusudi tuweze kumshitaki, tuweze kumshitaki kama akikiuka.

Itaendelea kesho...