Huduma za kidijitali NMB sasa kwa Kiswahili

Muktasari:

Benki ya NMB yaziweka huduma zake katika lugha ya Kiswahili kwa njia ya digitali, sasa huduma zote kupatikana kwenye simu ya mkononi kupitia NMB Mkononi


Dar es Salaam. Katika kuhakikisha huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi bila kujali kiwango chao cha elimu Benki ya NMB imeziweka huduma zake katika lugha ya Kiswahili.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni mpya ya benki hiyo ya kuhamasisha matumizi ya digitali katika kupata huduma za kibenki.

Ofisa Mkuu wateja binafsi, biashara ndogo na za kati Filbert Mponzi amesema kampeni hiyo inayofahamika kama ‘NMB Mkononi’ inalenga kuwafanya watanzania wa mijini na vijijini kutumia simu za mkononi kupata huduma za kibenki.

Mponzi ameeleza kuwa kupitia kampeni hiyo wateja wao wenye simu za mkononi hawatakuwa na ulazima wa kwenda kwenye matawi kwa ajili ya kupata huduma kwani kila kitu kinaweza kufanyika kwenye simu.

Kuhusu kutumia Kiswahili amesema utafiti umeonyesha kuwa asilimia 60 ya watumiaji huduma  hawana uwezo wa kuandika na kuzungumza lugha ya kiingereza hivyo wameona ni vyema kuwasogezea huduma zao kwenye simu za mkononi kwa kutumia lugha inayoeleka kwa watanzania wengi.

“Hivi  karibuni tumetoka kwenye mkutano wa SADC na lugha ya Kiswahili imepitishwa  lugha rasmi  mawasiliano, upande wetu tukaone tushiriki katika kuitangaza lugha hii na ndiyo maana tumesowasogezea watanzania hasa walioko vijijini waweze kupata huduma za kibenki kwa luga wanayoielewa,”

Huku mjini ukiwaambia watu mobile banking wanaweza kuelewa lakini vipi kuhusu kule vijijini ambako kuna watanzania nao pia wanahitaji kutumia simu zao kupata huduma za kibenki, tumeona tuiweke katika lugha ambayo itakuwa rahisi kueleweka na kutumika kwa yeyote anayefahamu kiswahili,” amesema Mponzi