VIDEO: Hukumu Mbowe na wenzake kutolewa Machi 10

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 10, 2020 kutoa hukumu ya kesi inayowakabili viongozi nane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 10, 2020 kutoa hukumu ya kesi inayowakabili viongozi nane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Dk Vicent Mashinji ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa Chadema. Dk Mashinji alihamia CCM Februari 18, 2020.

Katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kati ya Februari 1 na 16, 2018.

Uamuzi wa mahakama umetolewa leo Jumatatu Februari 24, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Pia Mahakama hiyo imetoa siku tano kwa mawakili wa pande zote kuwasilisha majumuisho kwa njia ya maandishi.

"Majumuisho ya pande zote mbili yanatakiwa kuwasilishwa Mahakamani hapa kwa njia ya maandishi katika siku tano za kazi kuanzia leo.”

"Kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa mashauri ya jinai pande zote zitakuwa na haki kisheria kuomba kufanya majumuisho ili kuweza kusaidia Mahakama kutoa uamuzi wake,” amesema Hakimu Simba

Hakimu huyo amebainisha kuwa Mahakama inaendelea kuchapa  mwenendo mzima wa kesi toka ilipoanza kwa ajili ya  kukabidhi kwa pande zote mbili.

Katika kesi hiyo Serikali ilifunga ushahidi kwa kuita mashahidi wanane huku upande wa utetezi ukiita mashahidi 13 wakiwemo washtakiwa wenyewe.

Mbali na Mbowe na Dk Mashinji, washtakiwa wengine ni katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.