KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Hukumu ya dakika 60 yawatia hatiani watano

Ndugu wa marehemu Erasto Msuya wakiangua kilio Jumanne Julai 23 katika viwanja vya Mahakama Kuu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kusomwa hukumu ya kesi ya mauaji ya Erasto Msuya. Washtakiwa watano walihukumiwa kunyongwa. Picha ndogo ni mshtakiwa namba mbili Shaibu Jumanne ‘Mredii’ aliyeachiwa huru katika kesi hiyo. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Hukumu hiyo imetoka wakati kesi ya Miriam Mrita, ambaye ni mke wa marehemu Msuya, ikitajwa jijini Dar es Salaam.
  • Miriam ameshtakiwa kwa tuhuma za kumuua dada wa mumewe ambaye ni maarufu kwa jina la Bilionea Msuya.

Moshi. Dakika 60 za hukumu ya kifo kwa washtakiwa watano wa mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na Arusha, Erasto Msuya, jana zilihitimisha kesi ya mauaji ya kukusudia iliyochukua miaka mitatu.

Hukumu hiyo imetoka wakati kesi ya Miriam Mrita, ambaye ni mke wa marehemu Msuya, ikitajwa jijini Dar es Salaam. Miriam ameshtakiwa kwa tuhuma za kumuua dada wa mumewe ambaye ni maarufu kwa jina la Bilionea Msuya.

Jijini Moshi, baada ya hukumu kusomwa, ndugu wa Bilionea Msuya akiwemo dada yake anayeitwa Antuja walijikuta wakibubujikwa machozi, huku wakiishukuru mahakama kwa maelezo kuwa imetenda haki.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 ambako pia lilikutwa gari lake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili.

Katika hukumu iliyosomwa na Jaji Salma Maghimbi kuanzia saa 3:40 asubuhi hadi saa 4:40 asubuhi Mahakama Kuu iliwahukumu adhabu ya kifo washtakiwa watano na kumuachia huru mmoja.

Waliohukumiwa kunyongwa ni Sharif Mohamed ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, Mussa Mangu (mshtakiwa wa tatu), Karimu Kihundwa (wa tano), (Sadik Jabir (wa sita) na Ally Majeshi ambaye ni mshtakiwa wa wa saba.

Jaji Maghimbi alimuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne, maarufu kwa jina la Mredii kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yake.

Akichambua ushahidi dhidi ya washtakiwa hao, Jaji Maghimbi alisema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo la washtakiwa wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono.

Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa na kusomwa mahakamani yalihusu mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Ally Majeshi.

Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, maelezo ya Sharifu ambayo yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, yanaeleza mpango mzima wa mauaji ulivyosukwa na bunduki ya SMG ilivyonunuliwa.

Pia katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo alieleza namna laini mpya za simu zilivyosajiliwa kwa majina ya Kimasai na namna pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo, zilivyonunuliwa.

Kuhusu mshtakiwa wa tatu, Jaji Maghimbi alisema ingawa katika maelezo yake ya kukiri kosa alianza kwa kujitoa na kuwabebesha mzigo washtakiwa wenzake, alishiriki katika nia hiyo ovu.

“Alijua mpango huo wa mauaji na akaendelea kushiriki katika mipango hiyo ya mauaji hadi mwisho bila kujitoa,” alisema Jaji.

“Kitendo cha kutojitoa katika mpango mzima wa mauaji kinaonyesha nia yake ovu ya kutenda kosa hilo. Hakufanya juhudi zozote za kujitoa katika mipango hiyo miovu ya mauaji,” alisema Jaji.

Jaji Maghimbi alisema maelezo ya Karim aliyeeleza kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi nyingi Msuya, yanaunganika na yake waliyoeleza Sharifu, Mussa na Majeshi.

Jaji Maghimbi alisema maelezo hayo ya kukiri kosa na maungamo ya washtakiwa, yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri na hivyo kuthibitisha shtaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavulla uliita mashahidi 27 waliotoa ushahidi kwa kuongea na watano ambao maelezo yao yalisomwa.

Chavulla ambaye alisaidiana na wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana na mawakili Ignas Mwinuka, Kassim Nassir na Lucy Kyusa pia waliwasilisha vidhibiti 26 vya kesi hiyo.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, wakili wa utetezi Majura Magafu aliiomba mahakama izingatie umri mdogo walionao washtakiwa na kwamba wamekaa muda mrefu gerezani na wanajutia kosa hilo.

‘Nimemuona Mungu’

Hukumu hiyo ilikuwa habari njema kwa ndugu wa Bilionea Msuya.

“Kwa kweli katika jambo hili nimemuona Mungu akitenda haki,” alisema Antuja Msuya, ambaye ni dada wa Bilionea Msuya.

“Nawashukuru wapelelezi makini waliopeleleza kesi hii. Zaidi ya yote namshukuru jaji aliyetoa hukumu hii.

“Kama familia nasema asante na tumeridhishwa na uamuzi huu.”

Antuja, huku akimiminika machozi na akibembelezwa na wenzake alishindwa kuendelea kuzungumza.

Baba mzazi wa marehemu, Simon Msuya pia aliishukuru mahakama, lakini akasema hakuridhishwa na hatua ya jaji kumuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne.

Jijini Dar es Salaam, jalada la kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Mrita, sasa lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita alisema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa jalada hilo linafanyiwa kazi na DPP.

Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala aliutaka upande wa mashtaka ufuatilie jalada hilo kwa kuwa sasa liko mikononi mwa DPP.

Katika kesi hiyo ambayo imeahirishwa hadi Julai 30, washtakiwa wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth Msuya, ambaye ni dada wa Bilionea Msuya, Mei 25, 2016 Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Mtiririko matukio ya kesi

Agosti 7,2013

Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

Agosti 11, 2013

Polisi inatangaza kukamatwa kwa washukiwa muhimu wakihusishwa na mtandao uliofanya mauaji hayo.

Agosti 21,2013

Watuhumiwa watatu, Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne na Mussa Mangu wanafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kujibu shtala la kumuua kwa makusudi Msuya.

Septemba 16, 2013

Kamanda wa Polisi Kilimanjaro wa wakati huo, Robert Boaz anatangaza kukamatwa kwa watuhumiwa wanne zaidi. Watuhumiwa hao ni Joseph Mwakipesile au Chusa (mfanyabiashara tajiri wa Mirerani), Sadick Mohamed, Karim Kihundwa na Jalila Said.

Septemba 18, 2013

Mwakipesile, Mohamed, Kihundwa na Said wanafikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji hayo.

Aprili 16, 2014

DPP anamfutia mashtaka Mwakipesile, akitumia kifungu na. 91 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai (CPA) ya 2002.

Juni 10, 2014

Upande wa mashtaka unawasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi 50 wa kesi hiyo na kutaja vielelezo vitakavyotumika.

Februari 10, 2015

Washtakiwa wanasomewa shtaka la mauaji ya kukusudia mbele ya Jaji Amaisario Munisi na wanakana kumuua Bilionea Msuya.

Oktoba 5, 2015

Kesi ya Bilionea Msuya inaanza kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu.

Mei 14, 2018

Jaji Maghimbi anamuachia huru mshtakiwa wa nne, Jalila Zuber baada ya kumuona hana hatia kulingana na ushahidi wa watu 32 wa mashtaka na vielelezo 26.

Ushahidi wa upande wa mashtaka

Mashahidi wa upande wa mashtaka walidai kuwa njama za kumuua Msuya zilianza Julai 2013 na watuhumiwa waliofanya mauaji waliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja.

lidaiwa kuwa katika kupanga mauaji hayo, simu mpya tano na laini tano zilisajiliwa kwa majina ya Kimasai, kununuliwa kwa pikipiki mbili na bunduki aina ya SMG.

Katika ushahidi huo, inadaiwa Majeshi ndiye aliyemvuta Msuya hadi eneo la tukio, akijifanya anataka kumuuzia madini ya Tanzanite.

Kulingana na maelezo ya ungamo ya Karim na ya onyo la kukiri kosa ya Majeshi, Karim ndiye aliyemfyatulia risasi mfanyabiashara huyo.

Katika ushahidi wake, Dk Paul Chaote aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Msuya alidai ulikuwa na majeraha 26 ya risasi yaliyosababisha mfumo wa damu na upumuaji kusimama.

Dk Chaote alidai kwa kuutazama kwa nje, mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha madogo 13 na makubwa 13 yaliyosababishwa na risasi zilizoingia mwilini na kutokea upande wa pili.

Alidai baada ya kuupasua mwili wa marehemu, walikuta utumbo mwembamba umekatika huku risasi hizo zikiharibu figo, mishipa ya damu na kupasua bandama.

Dk Chaote alidai mapafu yote mawili yaliharibiwa vibaya kwa risasi huku mishipa ya damu inayoingia kwenye mapafu, figo na bandama ikiwa imechakazwa vibaya kwa risasi.

Katika ushahidi wao, mashahidi wote waliegemea katika ushahidi wa mazingira ambao maofisa wa polisi walieleza namna washtakiwa walivyoshiriki tukio hilo na namna walivyowakamata.

Nyongeza na Tausi Ally, Dar es Salaam