IGP Sirro: Tunamtafuta Mwamposa

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro

Muktasari:

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania, Simon Sirro amemtaka Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa asisumbue vyombo vya dola kwa sababu anafahamika na ajisalimishe kituo chochote cha polisi kwa mahojiano na kuona usajili wake.

Dar es Salaam. Wakati Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro akisema  juhudi za kumtafuta na kumkamata Nabii na Mtume, Boniface Mwamposa zinaendelea, yeye tayari amewaaga waumini wake jijini Dar es Salaam leo kuwa anaelekea mkoani Kilimanjaro kuitikia wito wa Polisi.

Mapema leo asubuhi, IGP Sirro amesema wamemfuatilia Mwamposa bila mafanikio katika viwanja vya ndege na kama ametumia usafiri wa barabara jana kurejea Dar es Salaam.

Sirro alipohojiwa na Kituo cha luninga cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) amesema taarifa za awali, zilieleza kuwa Mwamposa  angeondoka kwa kutumia usafiri wa ndege usiku.

Na alikuwa aondokee Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA), lakini hakusafiri na ndege hiyo na walipofuatilia kwa njia ya barabara hawakumpata.

“Tumemfuatililia barabarani hatukumpata lakini juhudi zinaendelea, pia niwape pole wote waliofiwa na tuwaombee majeruhi wote wapone haraka,” amesema Sirro.

Mwamposa anatafutwa baada ya kutokea vifo vya watu 20 baada ya watu kukanyagana kwenye ibada ya kukanyaga mafuta ililofanyika jana Februari Mosi, 2020 katika viwanja vya Majengo vilivyopo wilayani Moshi mkoa wa Kilimanjaro.

Sirro ametoa angalizo kwa wananchi kuwa makini na makanisa kwa sababu yanazidi kuongezeka na amesema watazungumza na kamati za ulinzi na usalama za mikoa kupitia makanisa kuona kama zinafuata kanuni na taratibu wanazopewa wakati wa usajili.

“Haya yanatokea ila kuna cha kujifunza sio kila padre au mchungaji anataka kuwachunga watu wake kufika ufalme wa mbingu, wengine sitaki kuwahukumu ila wanahangaikia maisha yao ya hapa duniani,” amesema Sirro

Sirro amemtaka Mwamposa asisumbue vyombo vya dola kwasababu anafahamika na ajisalimishe kituo chochote cha polisi kwa mahojiano na kuona usajili wake.

Kuhusu suala la ulinzi wa polisi wa eneo husika IGP Sirro amesema ameshawasiliana na Kamanda wa Polisi Kilimanjaro, Salum Hamduni kufuatilia kama kuna uzembe ulikuwepo na tayari uchunguzi unaendelea.