Idadi ya wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi imepungua

Wageni waalikwa wakisoma kitabu cha hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ilipokuwa ikiwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Baada ya kuimarisha huduma za afya nchini, Serikali imesema idadi ya wanaoenda kutibiwa nje ya nchi imepungua.


Dar es Salaam. Serikali imesema idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipelekwa kutibiwa nje ya nchi imepungua hivyo kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kwa ajili hiyo.

Akielezea mafanikio ya Serikali alipokuwa anasoma Bajeti Kuu ya mwaka 2019/20 leo June 13, 2019, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema kuimarisha upatikanaji wa dawa, vitenganishi na huduma za kibingwa nchini kumechangia pa kubwa kupungua kwa wagonjwa wanaosafirishwa.

Waziri huyo amesema mbali na mafanikio hayo, Serikali imeboresha huduma za afya katika hospitali za mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati .