Iraq washangilia tangazo la Mahdi kujiuzulu

Muktasari:

Waandamanaji washangilia huku wengine wakitaka mabadiliko zaidi katika mfumo mzima wa uongozi wa nchi.

Baghdad, Iraq. Umati uliofurika jana katika eneo maarufu la kimapinduzi, Tahrir Square mjini Baghdad umelipuka kwa shangwe, nderemo na vifijo kufuatia taarifa kwamba Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul Mahdi atawasilisha kwa Bunge barua ya kujiuzulu wadhifa huo.

Uamuzi huo wa Mahdi umefikiwa baada ya umwagaji mkubwa wa damu ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya Iraq kwa vitendo vya rushwa, ukosefu wa ajira na kudorora kwa huduma za jamii.

Hata hivyo, wakati wengi wakifurahia hatua hiyo, baadhi ya waandamanaji walibaki na wasiwasi, wakitaka mabadiliko ya mfumo mzima wa uongozi wa kisiasa.

Kutokana na mtazamo huo, maandamano yameendelea mjini Baghdad na maeneo mengine nchini, waandamanaji wakisema “mafisadi wote wajiuzulu”.

Barua ya kujiuzulu

Jana Ijumaa, Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul Mahdi alisema angewasilisha kwa Bunge barua yake ya kujiuzulu nafasi hiyo baada ya kutokea umwagaji mkubwa wa damu kwa waandamanaji wanaoipinga Serikali.

Uamuzi wa Mahdi ulitolewa katika taarifa hiyo kufuatia wito wa kutaka mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi hiyo, uliotolewa na Kiongozi wa Madhehebu ya Shia nchini humo, Ayatollah Ali al-Sistani.

“Nitawasilisha barua ya kujiuzulu kwa Bunge kutoka wadhifa wa waziri mkuu ili Bunge liweze kufanya linachoweza kufanaya,” alisema.

Awali, Al-Sistani alisema Bunge lililoichagua serikali ya Mahdi yenye mwaka mmoja madarakani, linatakiwa “kuangalia jambo la kufanya”.

“Tunatoa wito kwa Bunge ambalo hii serikali ilitokea kuangalia namna ya kufanya kuhusu hili, Al-Sistani alisema katika mawaidha yake ya wiki katika mji mtakatifu wa Najaf, kupitia mwakilishi wake.

Abdul Mahdi alisema “nimesikiliza kwa umakini sana mawaidha ya Sistani na nimeamua kuitikia wito wake kwa kwa ukamilifu haraka iwezekanavyo.”

Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya zaidi ya watu 50 kuuawa na vikosi vya serikali, siku ambayo ni ya umwagaji mkubwa wa damu kuwahi kushuhudiwa tangu maandamano ya kuipinga serikali yaanze mapema Oktoba.

Tangu mwezi Oktoba, idadi ya watu iliyoripotiwa kuuawa katika maandamano hayo ni 400.