Isemeeni Serikali mazuri inayofanya, msiwakalie kimya wapotoshaji – Dk Possi

Friday December 6 2019

By Rachel Chibwete, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo nchini Tanzania, Dk Ally Possi amewataka maofisa mawasiliano wa Serikali nchini humo, kuelezea mazuri yanayofanywa na serikali yao hususan katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa, badala ya kuwaacha watu wanapotosha ukweli.

Dk Possi ametoa kauli hiyo leo  Ijumaa Disemba 6, 2019 wakati akifunga mafunzo kwa maofisa mawasiliano hao kutoka sekta mbalimbali nchini.

Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amewataka kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kuweka mambo mazuri yanayofanywa na serikali hasa kwenye miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini, kwa kuwa ndiyo jukumu lao la kuhabarisha umma.

“Tumieni mitandao kutoa taarifa kwa umma kuhusu miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini badala ya kuwaacha mabepari ambao wanapotosha umma kwa kutumia hiyohiyo mitandao na kama mnavyojua habari ya uongo husambaa kwa haraka,” amesema Dk Possi.

“Ni jukumu lenu kutoa habari na taarifa kwa umma za kweli na kwa wakati ili Watanzania wajue kinachoendelea kuliko kukaa kimya na kuwaacha wapotoshe ukweli,” amesema.

Advertisement

Amewataka wasijidharau mbele ya watu hata kama wana majina au vyeo vikubwa, bali watekeleze majukumu yao kwa weledi kwa kuwa taaluma yao ni nyeti na inaweza kumwinua mtu au kumshusha kulingana na atakavyoandikwa na wao.

Pia, amewataka waitumie taaluma yao vizuri kwa kuandika habari zinazojenga nchi, kuleta umoja, mshikamano na utulivu badala ya kuandika taarifa za uchochezi ambazo zitalitumbukiza Taifa kwenye machafuko na vita.

Makamu mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini (TAGCO), Sara Masika amesema mafunzo hayo ya siku tano yalilenga kuwajengea uwezo wa jinsi ya kufanya kazi zao kwa weledi hasa kwa kutumia mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma masuala mbalimbali yanayoendelea.

Advertisement