Itakachokifanya ACT- Wazalendo ikiingia Ikulu 2020

Muktasari:

  • Leo Jumamosi Machi 14, 2020 Chama cha siasa za upinzani nchini Tanzania cha ACT- Wazalendo kinafanya mkutano mkuu wa pili katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam ambapo mbali na mambo mengi watafanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi watakaokiongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo nchini Tanzania, Zitto Kabwe amesema chama hicho kikipata nafasi ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktiba 2020 kitahakikisha uchumi wa nchi unakua kwa asilimia 11 pamoja na kujenga uchumi jumuishi na kuimarisha pato la Mtanzania.

Mbali na hilo, amesema atahakikisha anapunguza ukosefu wa ajira kwa watu wengi na kugusa sehemu za kiuchumi zinazotegemewa na watu wengi.

Zitto ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 14, 2020 katika  mkutano mkuu wa pili wa chama hicho unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

Amesema chama hicho kitakaposhika nchi kinataka kuonyesha tofauti na kile kulichokuwa madarakani kwa muda mrefu cha CCM huku akibainisha watahakikisha wanaongoza Serikali itakayotekeleza sera sahihi zitakazojenga uwezo wa kufaidika zaidi na rasilimali watu.

“Tukiongoza serikali na tukatoka madarakani mwaka 2030 Tanzania tunayotaka kuiacha ni ile ambayo uchumi wa Tanzania unakuwa kwa asilimia 11 kwa mwaka, kupunguza ukosefu wa ajira hadi chini ya asilimia 3 pamoja na kupunguza umasikini hadi kufikia walau asilimia 5 kutoka 28 ya sasa.”

“Pia, kila Mtanzania atakuwa na bima ya afya na siyo vifurushi vya bima vinavyotajwa sasa,” amesema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini

Amesema hayo yote yatafanikiwa kupitia kauli mbiu yao ya kazi na bata ambayo itampatia Mtanzania uhuru wa kufanya kazi halali, kupata kipato chake na kukitumia atakavyo.

Zitto amesema baada ya kuingia madarakani watahakikisha nchi unawekeza zaidi katika shughuli za wananchi wengi ikiwamo kilimo hasa kile cha umwagiliaji, uvuvi na ufugaji

“Lengo la haya yote ni kutaka kuongeza shughuli za kiuchumi kwa watu kwa sababu uchumi wa watu ndiyo unajenga Taifa imara na sio uchumi wa Serikali,” amesema Zitto