Jafo atangaza Agosti 7 kuwa siku ya lishe Tanzania

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi),  Selemani Jafo ametangaza Agosti 7 kila mwaka kuwa siku ya lishe Tanzania

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi),  Selemani Jafo ametangaza Agosti 7 kila mwaka kuwa siku ya lishe Tanzania.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 24, 2019 jijini Dodoma wakati akizungumza na wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wataalam wa lishe kwenye mkutano wa tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe nchini.

Kwa mujibu wa Jafo, bila kumaliza tatizo la udumavu kwa kutoa elimu ya lishe, tatizo litakuwa kubwa siku za usoni.

Ametoa sababu za kupanga siku hiyo ni kwa kuwa inaangukia sikukuu ya wakulima Nanenane, watu wengi huitumia kwa ajili ya maonyesho ya bidhaa za kilimo.

"Siku hii haitawasumbua kwa kuwa inaangukia siku ya wakulima, hapa tutaonyesha bidhaa za kilimo ambazo ni muhimu ili tupambane na adui udumavu," amesema Jafo.

Ameagiza ikifika Septemba 30, 2019 kila kijiji na kata nchini viwe vimesaini mkataba katika shughuli za lishe na kuwataka waganga wakuu wa Mikoa kusimamia pamoja na vituo vya afya kufanya kazi.