VIDEO: Jafo awataka makatibu tawala kutenda haki uchaguzi Serikali za mitaa

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amewataka makatibu tawala nchini Tanzania kutenda haki kwa vyama vyote vya siasa katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.


Babati. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo amewataka makatibu tawala nchini Tanzania kutenda haki kwa vyama vyote vya siasa katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Amesema makatibu tawala hao ambao ni wenyeviti wa kamati za rufaa kwenye mchakato wa uchaguzi huo kuhakikisha wagombea wote wenye malalamiko wanasikilizwa.

Jafo ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 6, 2019 mkoani Manyara katika kikao cha tathmini ya mchakato wa uchaguzi huo mkoani humo.

Amesema viongozi hao wanatakiwa kutoa uamuzi bila hofu yoyote.

Amebainisha kuwa vyama vitakavyoona havijatendewa haki,  wagombea wake wanatakiwa kukata rufaa katika kamati hizo.

"Nyinyi kazi yenu ni kusimamia vyama vilivyokata rufaa na kutoa haki, msimuonee aibu wala kumuogopa mtu katendeni haki kwa wote watakaoleta malalamiko yao," amesema Jafo.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema wagombea wa CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo walichukua fomu na kurudisha fomu.

“Kwenye Mkoa wetu hakuna mgombea wa chama chochote aliyewekewa mizengwe, aliyenyimwa fomu au ofisi kufungwa, kasoro zilizopo ni wagombea wenyewe kukosea kujaza fomu," amesema Mnyeti.