Jafo azijibu balozi za Marekani, Uingereza

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo


Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amefafanua kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita uliendeshwa kwa haki akijibu tamko la nchi za Marekani na Uingereza ambazo zimeukosoa.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amefafanua kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita uliendeshwa kwa haki akijibu tamko la nchi za Marekani na Uingereza ambazo zimeukosoa.

Jafo, ambaye ofisi yake ilisimamia uchaguzi huo, aliiambia Mwananchi jana kuwa mchakato wote ulifuata kanuni na sheria za nchi.

Balozi za Marekani na Uingereza nchini, jana zilitoa tamko zikikosoa uchaguzi huo wa serikali za mitaa zikidai haukuwa huru, haukuendeshwa kwa haki na kutengwa kwa wapinzani.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, mitaa yote nchini 4,263 sawa na asilimia 100 na vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4.

Akizungumzia tamko la mataifa ya Marekani na Uingereza, Jafo alisema kwa mujibu wa maadili ya kazi yake hana mamlaka ya kujibu suala hilo isipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi ingawa alitoa maelezo ya kutetea mchakato huo.

“Sina sababu ya kujibu kwa sababu maadili hayaniruhusu isipokuwa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mujibu wa taratibu za kazi. Ila ninachojua uchaguzi ulikuwa wa haki na ulifanyika kwa mujibu kwa kanuni na sheria za nchi.

“Huo ni mtazamo wao (nchi za Marekani na Uingereza), sisi tuliendesha uchaguzi vizuri kwa kufuata kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa za mwaka 2019,” alieleza Jafo.

Jafo alisema uchaguzi huo ulikuwa wa kidemokrasia hakukuwa na mashaka yoyote ndio maana baadhi ya vyama vya upinzani vilitangaza kujitoa katika mchakato huo kwa sababu mbalimbali ingawa baadhi ya wagombea wao wa nafasi mbalimbali waligoma kujitoa,” alisema.

Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzani vya Chadema, UPDP, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD, Chauma na ACT-Wazalendo vilijitoa kwa kile walichodai kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato huo na kulalamikia wagombea wao kutotendewa haki.

Hata hivyo, vyama vya DP, Ada Tadea, NRA, TLP, AAFP vilishiriki uchaguzi huo vikidai sababu zilizotolea na viongozi wa vyama vilivyojitoa hazikuwa na mashiko.

“Ni kweli wapinzani walijitoa lakini baadhi ya wagombea wao hawakukubaliana na hali hii, waligoma kujitoa katika mchakato huu. Mfano mzuri katika wilaya ya Nkasi (Rukwa), Chadema imepata vijiji viwili,” alisema Jafo.

Tamko la Marekani, Uingereza

Nchi za Marekani na Uingereza jana zilitoa matamko ya kuelezea kusikitishwa na mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa nchini.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa taarifa ya kueleza kusikitishwa na uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita ikisema kwa kiasi kikubwa wasimamizi wa uchaguzi huo waliwatenga wagombea wa upinzani.

“Hali hii ya mkanganyiko inazua swali kuhusu uhalali wa mchakato huu wa uchaguzi na matokeo yake. Msimamo wa Serikali wa Tanzania kukataa kutoa vibali kwa wakati kwa waangalizi wanaokubalika na mashirika yenye uzoefu kunapoteza imani katika mchakato mzima,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani.

Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke alieleza msimamo wake wa kukosoa uchaguzi huo kupitia mtandao wa kijamii wa twitter.

“Tumetatizwa na namna uchaguzi wa serikali za mitaa ulivyoendeshwa. Kutokana na kukosekana kwa waangalizi wa ndani kwenye mchakato huo, kuenguliwa kwa wagombea wa upinzani na kujitoa kwa baadhi ya vyama,” alisema balozi Cooke kwenye taarifa yake fupi jana.

Balozi Cooke alisema kujitoa kwa baadhi ya vyama maana yake kulikosesha Watanzania fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa njia ya haki.