Jafo kumkabidhi Magufuli majina ya wakurugenzi wavivu

Muktasari:

Waziri wa nchi Tamisemi, Seleman Jafo amesema ana majina ya wakurugenzi wasiokwenda na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania, atayakabidhi kwa Rais John Magufuli Aprili, 2020.

Dodoma. Waziri wa nchi Tamisemi, Seleman Jafo amesema ana majina ya wakurugenzi wasiokwenda na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania, atayakabidhi kwa Rais John Magufuli Aprili, 2020.

Jafo ameeleza hayo leo Jumatano Januari 22, 2020 mjini Dodoma wakati akikabidhi mashine 7227 za kukusanyia mapato kwa halmashauri zote.

Mashine hizo imetolewa  na balozi wa Norway nchini Tanzania,  Elisabeth Jacobsen.

Waziri huyo amesema ameshindwa kuzivumilia baadhi ya halmashauri  kwa kuwa zinatekeleza majukumu yake kinyume na miongozo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kutokusanya fedha ipasavyo.

"Wiki ijayo nitatoa taarifa ya makusanyo yote kwa halmashauri, lakini taarifa yangu ya mwezi Aprili  nitaorodhesha majina na kumkabidhi mwenye mamlaka, nitatoa mapendekezo ikibidi wakurugenzi waachiwe maana hawatufai," amesema Jafo.

Amebainisha kuwa kuna halmashauri zinadaiwa madeni makubwa, zikiwemo posho za madiwani, “kuna halmashauri inadaiwa Sh758 bilioni ambazo ni malimbikizo ya posho za wabunge, mkurugenzi wake anapaswa kujitathimi.”