Jaji asema kusimamishwa kuapishwa mbunge wa CCM hakuathiri maombi ya Lissu

Muktasari:

  • Mahakama Kuu nchini Tanzania  imesema ombi la kusimamishwa kuapishwa kwa  mbunge mteule wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu haliwezi kutolewa leo Jumatatu Septemba 2, 2019.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu nchini Tanzania  imesema ombi la kusimamishwa kuapishwa kwa  mbunge mteule wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu haliwezi kutolewa leo Jumatatu Septemba 2, 2019.

Hayo yameelezwa leo saa 2:48 usiku na Jaji Sirillius Matupa  kuhusu maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ya kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu kukoma kwa ubunge wake.

Jaji huyo amesema kwenye kesi za ubunge hata kama mtu ameapishwa anaweza kuvuliwa ubunge pamoja na kiapo chake.

Kutokana na uamuzi huo, ratiba ya kuapishwa kwa mbunge huyo inaweza kuendelea kesho bungeni mjini Dodoma ambako vitaanza vikao vya mkutano wa 16 wa chombo hicho cha kutunga sheria.

Jaji Matupa amesema maombi rasmi ya Tundu Lissu kupinga mambo kadhaa kuhusu kuondolewa katika ubunge yatatolewa Septemba 9, 2019.

Lissu amefungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Spika wa Bunge awasilishe mahakamani taarifa ya kumvua ubunge aliyoitoa bungeni ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Nyingine ni mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya  kusitishwa kuapishwa kwa Mtaturu.

Mwanasheria mkuu huyo wa  Chadema yuko nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu baada ya Septemba 7, 2017 kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana akiwa katika makazi yake, mjini Dodoma akiwa ametokea bungeni.

Juni 28, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu huku akisema si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya katiba ya nchi.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutohudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi kueleza mahali alipo na kutotoa taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.