Jalada tuhuma zinazomkabili Idriss Sultan latua kwa DPP

Muktasari:

  • Jalada la uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili msanii wa vichekesho nchini Tanzania, Idris Sultan limepelekwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP).

Dar es Salaam. Jalada la uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili msanii wa vichekesho nchini Tanzania, Idris Sultan limepelekwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP).

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 13, 2019 na Benedict Ishabakaki ambaye ni mwanasheria wa msanii huyo.

Idris anadaiwa kusambaza habari za uongo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao na kujifanya Rais chini ya kifungu cha 15 cha makosa ya mtandao.

Ijumaa Novemba Mosi, 2019 Idris aliripoti kituo cha polisi kati baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda alichukua uamuzi huo baada ya msanii huyo kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais wa Tanzania, John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani.

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Tangu Novemba Mosi hadi sasa Idris amesharipoti polisi zaidi ya mara tatu lakini leo mwanasheria huyo akisema tayari uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili umemalizika baada ya kuripoti polisi na kuelezwa suala hilo.

“Tulipofika tuliambiwa tayari upelelezi kwa Polisi umekamilika na jalada wameshalipeleka kwa DPP.”

“Huko ndio tutajua hatma kama mteja wetu atatakiwa kufikishwa mahakamani au la. Jibu tunatarajia kulipata Jumatatu Novemba 18, 2019,” amesema mwanasheria huyo.

Ilivyokuwa

Mkasa ulianza kama masihara kwa Idris kuweka katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram picha yenye sura yake akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa huku akiandika “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani.”

Baada ya kuweka picha hiyo, Makonda alichangia katika mtandao huo na kumtaka mchekeshaji huyo wa vituko vya ‘Sio Habari’ kujisalimisha polisi.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”

Alipozungumza na Mwananchi baadaye kuhusu sakata hilo, Makonda alisema “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”

Kuhusu hatua ya Dk Kigwangalla kumwekea dhamana Idris iwapo atakamatwa, Makonda alisema “brother ile Twitt sikumuandikia mtu yeyote zaidi ya Idris, nenda kaisome vizuri.”