James Bond 'halisi' afariki

Muktasari:

Sean Connery alielezewa na mashabiki wa filamu kuwa ndiye muigizaji bora wa nafasi ya James Bond, akiwaacha mbali wasanii wengine kama 007 wa sasa Daniel Craig na Roger Moore.

 

London, Uingereza (AFP). Wasanii tofauti wameigiza nafasi ya James Bond katika filamu kadhaa, lakini mcheza sinema gwiji, Sean Connery, ndiye aliyecheza nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.

Sasa hayupo tena duniani baada ya kufariki dunia akiwa na miaka 90.

Jason Connery, mtoto wa kiume wa nyota huyo aliyependwa na Waingereza wengi, amesema baba yake alifariki kwa amani akiwa usingizini mjini Nassau katika visiwa vya Bahamas, ambako ana nyumba yake, baada ya hali yake kutokuwa nzuri kwa muda mrefu.

"Wote tunafanyia kazi kuelewa tukio hili kubwa kwa kuwa ndio kwanza limetokea," aliongeza, akielezea kifo cha baba yake kuwa ni "pigo kwa watu wote duniani ambao walifurahia zawadi aliyokuwa nayo kama muigizaji".

Hafla ya heshiamza mwisho kwa Connery itakayofanyika baadaye, kwa mujibu wa ofisa habari wake.

Mcheza filamu huyo, ambaye pia alipewa na malkia wa Uingereza heshima ya kuwa Sir mwaka 2000, alitwaa tuzo kadhaa wakati wa kipindi cha uigizaji wake  kilichodumu kwa miongo, zikiwemo tuzo za Oscar, Golden Globes na Bafta.

Lakini ilikuwa ni sinema maarufu ya 007, aliyoigiza akitumia Kiingereza chenye lafudhi ya Scotland akiigiza kama mpelelezi aliyekuwa na leseni ya kuua, iliyompatia umaarufu mkubwa duniani kote.

Alikuwa ni muigizaji wa kwanza kutoa maneno yasiyosahaulika ya "Bond, James Bond" na aliigiza filamu sita zilizotokana na mtunzi wa vitabu vya hadithi, Ian Fleming.

"Alikuwa na siku zote ataendelea kukumbukwa kama James Bond halisi," walisema watayarishaji filamu maarufu, Michael G. Wilson na Barbara Broccoli.

Mara kadhaa , mcheza sinema huyo kutoka Scotland alipigiwa kura na mashabiki ya kuwa muigizaji bora wa nafasi ya Bond, akiwashinda waigizaji wengine kama Daniel Craig wa sasa na Roger Moore.