January, Nape waibua mjadala mitandaoni

Muktasari:

  • Wabunge na mawaziri wa zamani wameandika ujumbe kwenye akaunti zao za Twitter bila kufafanua jambo lililoibua mjadala kwa wachangiaji wa mtandao hao.

Dar es Salaam. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Nape Nnauye (Mtama) na January Makamba (Bumbuli) wameibua mjadala kutokana na ujumbe walioandika katika akaunti zao za Twitter.

Nape na Makamba ambao walikuwa mawaziri, wamewekwa kando kwa nyakati tofauti na kwa siku za hivi karibuni wamekuwa na mvuto kwa macho ya Watanzania wengi.

Mvuto huo umeongezeka zaidi baada ya siku za hivi karibuni kumuomba radhi Rais John Magufuli kutokana na kuvuja kwa mazungumzo yao ya simu waliyokuwa wakimteta mkuu huyo wa nchi.

Leo, Septemba 15, 2019, Nape aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter: “Nikumbushe wema wako nisije laumu, nikumbushe ukuu wako wakati wa magumu, nikumbushe shuhuda zako ili nikusifu…niimbie sifa katikati ya machozi.”

Wakati Nape akiandika hayo, Makamba aliyekuwa waziri wa muungano na mazingira ameandika: People who are real never broadcast that they are real.” (Watu ambao ni wa kweli kamwe hawatangazi kuwa wao ni wa kweli).

akichangia ujumbe huo, Isack Mackphason @mackphason amesema, “lakini kupiga magoti wanaweza.”

Akijibu ujumbe huo, Makamba amesema,  sio magoti tu, hata kutambaa kwa tumbo kama nyoka.

Akichangia ujumbe huo wa Makamba, @MzeeMaarifa ameandika:  “Ha ha ha hili dongo lako January ni funga kazi hongera kwa uungwana wako. Nakuhusudu sana mdogo wangu kweli sasa umekomaa kisiasa nakuombea, mola azidi kutuhudumia Watanzania kwa moyo wa dhati na Mungu anakuona na hakika atakulipa.

Wachangiaji wengine walikuwa @Salumkatemba aliyeandika: “naona picha za kihindi zikipita” na @MasoudJr akasema: “brother  wakati mwingine siyo lazima ujibu huku.”

Wakijibu ujumbe wa Nape, @glassamo ameandika “hahaha. Ukumbushwe wema wake, kwani alikufanyia baya gani?” Na @Justinswai3 akaandika “umeanza mashairi mzee baba baada ya kujifunga.”

Wachangiaji wengine walisema tofauti, @Zoharimohamed ameandika “kila la kheri na endelea kufanya ibada kila palipo na uzito patakua pepesi” wakati @Lumolakahumbi ameandika “kaka baada ya kuchomoa betri ndio umekuja na hii.”

Hata hivyo, @DizoClassic amemjibu Nape kwa kuandika “Mh...inapendeza sana ninapoona kiongozi akitumia hata sekunde moja kuzungumza na #Mungu maana najua ukaribu wa #mwanadamu na #Mungu huzaa imani na utu, upendo, pia ukweli uwazi na uongozi bora.                                             

@Stanjacks amesema “ikawa jion kisha asubuhi siku nyingne tena” huku @SylvesterMavanza akisema inapendeza sana hasa inapokuwa bila unafiki. "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna." - Wagalatia 6:7” wakati @Why So Serious? aliandika “Na Mola hakuishia hapo katika Yeremia 17:5 Bwana asema hivi," Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana."