Jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka nane

Muktasari:

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemuhukumu, Stambuli Yusufu (35) kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia ya kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kike wa miaka nane.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemuhukumu, Stambuli Yusufu (35) kifungo cha maisha jela baada ya kumkuta na hatia ya kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kike wa miaka nane.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kumfanyia kitendo hicho mtoto huyo anayesoma darasa la nne kati ya mwaka 2017 na 2018.

Imeelezwa kuwa baada ya kitendo hicho alikuwa akimpatia Sh1,000  hadi 2,000, kumtaka asiseme kwa mtu yeyote.

Akisoma hukumu hiyo leo Jumanne Januari 28, 2020 hakimu mkazi, Jimson Mwankenja amesema kifungo cha maisha jela kitaanza kuhesabiwa  baada ya mshtakiwa  kumlipa Sh2 milioni  mtoto huyo.

Amesema ikiwa atashindwa kulipa fidia hiyo, atachapwa viboko 12 na kuanza kutumikia kifungo hicho.

Hakimu Mwankenja amesema ametoa hukumu hiyo baada ya kuzingatia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka, utetezi wa mshtakiwa na uzito wa kosa hilo.

Baada ya kutoa hukumu hiyo, Hakimu Mwankenja alitoa somo kwa mawakili wa upande wa mashtaka kuwajibika kwa kuainisha vifungu vya sheria kwa ufasaha kwenye hati za mashtaka.

Amesema katika kesi hiyo, kwenye hati ya mashtaka waliandika kifungu cha 154(1) na (2) bila ya kuainisha kama kilifanyiwa marekebisho  na kifungu cha 16 cha makosa ya kujamiiana namba 4 ya 1998.