Jenerali Kayihura wa Uganda apigwa ‘stop’ kuingia Marekani

Aliyekuwa mkuu wa polisi wa Uganda Jenerali Kale Kayihura

Washington. Serikali ya Marekani imempiga marufuku kuingia nchini humo aliyekuwa mkuu wa polisi wa Uganda Jenerali Kale Kayihura pamoja na familia yake.

Marekani imesema ina taarifa za kuaminika kwamba Kayihura, ambaye alikuwa mkuu wa polisi wa Uganda kati ya mwaka 2005 na 2018, alihusika katika ukandamizaji wa haki za kibinadamu.

Taarifa iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo na kunukuliwa na sauti ya Amerika (VOA), Jenerali Kayihura alihusika moja kwa moja katika kuwatesa raia wa Uganda, kwa kuunda kikosi maalumu katika jeshi la polisi kilichopata amri ya moja kwa moja kutoka kwake na kuwadhulumu raia hao wakati wa uongozi wake.

Kulingana na sheria za kimataifa za Marekani, Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani inapokuwa na taarifa za kuaminika kuwahusu maofisa katika serikali za nje, wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi, au ukandamizaji wa haki za binadamu, maofisa hao na watu wa familia zao wanapigwa marufuku kuingia Marekani.

Mke wa Kayihura, Angela Umurisa Gabuka, binti wake Tesi Uwibambe na mtoto wake wa kiume Kale Rudahigwa nao pia wamepigwa marufuku kuingia Marekani.

Serikali ya Marekani imesema hatua dhidi ya Kayihura inatokana na wasiwasi wa kuendelea kwa ukandamizaji wa haki za kibinadamu nchini Uganda na kutaka serikali ya Yoweri Museveni kuheshimu haki za kibinadamu, uhuru wa raia wake na kuwapa uhuru wa kuandaa mikutano ya umma kwa njia ya amani.

Agosti mwaka jana, Jenerali Kayihura alifunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi jijini Kampala, akihusishwa na matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo kushindwa kulinda silaha za kijeshi na kusaidia katika utekaji nyara.

 

Kayihura (63) alikuwa anatuhumiwa kwa kuwaruhusu watu ambao si maafisa wa usalama, kama wanachama wa kundi la wahudumu wa boda boda 2010, likiongozwa na Abdullah Kitata kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria, wakati wa uongozi wake wa miaka 13 kama mkuu wa polisi.

Wasimamizi wa mashtaka wakiongozwa na Meja Jenerali Mugisha wamliiambia mahakama kwamba Kayihura alishindwa kutoa hesabu kamili ya bunduki na risasi zilizo katika kila kituo cha polisi na idara zote za usalama.

Vyombo vya habari vya Uganda viliripoti wakati huo kwamba bunduki 4,000 zilikuwa zimepotea wakati wa utawala wa Kayihura, lakini msemaji wa polisi Emilian Kayima alikanusha taarifa hizo akisema hazikuwa na ukweli wowote.