Jenerali Mabeyo awataka wanajeshi kulinda afya zao

Muktasari:

  • Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amewataka wanajeshi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ili kuipunguzia Serikali gharama za matibabu.

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amewataka wanajeshi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ili kuipunguzia Serikali gharama za matibabu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 23, 2019 wakati wa uzinduzi wa kitengo cha figo katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.

CDF Mabeyo amesema magonjwa ya figo yanaigharimu Serikali fedha nyingi, kwa muda mrefu wanajeshi na familia zao wamekuwa wakitibiwa ndani na nje ya nchi.

“Tukizingatia kanuni za afya tutalipunguzia Taifa gharama za matibabu, si wanajeshi pekee ugonjwa huu umekuwa ukitugharimu sana lazima tufahamu kuwa utumishi wa mwanajeshi hutegemea afya nzuri,” amesema Mabeyo.

Amesema Rais John Magufuli alitoa Sh431 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kitengo hicho mwaka 2017, kwamba kukamilika kwa ujenzi huo kulianzisha mchakato mwingine wa ununuaji wa mashine za kuchuja damu kwa wagonjwa wa figo (dialysis).

“Hiki ni kitengo cha kwanza kuanzishwa nchini tangu jeshi lilipoanzishwa mwaka 1964, tulianza ujenzi mwaka 2016 mpaka 2017 tulikamilisha na hapo ikabidi tuangalie namna gani tutapata fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa, mashine hizi tumezinunua kwa Sh633 milioni,” amesema.

Dk Mwinyi amesema wanajeshi hawatahitaji fedha nyingi kupata matibabu katika kitengo hicho na kwamba Serikali itaendelea kukijengea uwezo kuendana na teknolojia.