Jeshi Uganda lafanya mabadiliko ya sare zake

Muktasari:

Mavazi hayo ikiwamo kofia yanafanana na zile zinazovaliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo chini ya vugu vugu la Peoples Power linaloongozwa na mbunge na msanii, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Kampala Uganda. Jeshi la uganda (UPDF), limefanya mabadiliko katika sare zake za kijeshi katika vikosi mbali mbali na kutangaza katika gazeti rasmi la Serikali.

Hatua hiyo ilitangazwa jana Jumatatu Septemba 30 baada ya kuidhinishwa Septemba na Baraza la Kijeshi Septemba 18, mwaka huu.

Mavazi hayo ikiwamo kofia yanafanana na zile zinazovaliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo chini ya vugu vugu la Peoples Power linaloongozwa na mbunge na msanii, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Hata hivyo, wafuasi hao wameapa kuendelea kuvaa mavazi ya vugu vugu lao licha ya tangazo hilo la UPDF.

Gazeti la The Daily Monitor la Uganda limeandika kuwa, kwa mujibu wa sheria hiyo mtu yoyote atakayevaa sare za jeshi atafunguliwa mashtaka katika Mahakama ya kijeshi.

Kwa muda mrefu mwanasiasa huyo pamoja na wafuasi wake wamekua wakivaa kofia nyekundu kama na kudai kuwa ina maana ya ‘nembo ya uasi’.

Japo Bobi Wine hajatoa tamko lolote kuhusiana na sheria hiyo mpya lakini baadhi ya viongozi wa waandamizi wa vugu vugu la People Power wameliambia Shirika la habari la AFP kwamba wataendelea kuvaa kofia hizo.

"Tutaendelea kuvaa kofia zetu nyekundu," alisema kiongozi wa vijana Ivan Boowe. "Hakuna mtu atakayetutisha wala kututia uoga kwa kupigania haki yetu."

"Kwa kujumuisha kofia yetu katika sare za kijeshi, Serikali inapanga njama ya kupiga marufuku vugu vugu la People Power na tuko tayari kukabiliana na hatua itakayotekelezwa na serikali,"aliongeza.