Jeshi la Magereza Tanzania kuanzisha kiwanda cha mikate

Muktasari:

Jeshi la Magereza nchini Tanzania limesema katika mwaka wa fedha 2020/21 linakusudia kuanzisha kiwanda cha mkate kitakachojengwa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga jijini Dar es Salaam.

Dodoma. Jeshi la Magereza nchini Tanzania linatarajia kuanzisha kiwanda cha Mikate kitakachojengwa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 20, 2020  na Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Jeshi hilo, Ambayuu Kitiku wakati akiwasilisha maelezo ya randama kuhusu makadirio ya mapato, matumizi ya kawaida na miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2020/2021 mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

“Katika mpango wa bajeti wa mwaka 2020/2021 jeshi limeweka vipaumbele katika maeneo ya ajira na maendeleo ya watumishi, utawala wa magereza, uboreshaji miundombinu ya majengo ya magereza, kuimarisha shughuli za kilimo ili kujitosheleza kwa chakula.”

“Kuimarisha shughuli za Shirika la Magereza na kuimarisha shughuli za viwanda ikiwapo ujengaji wa kiwanda cha Mikate kitakachojengwa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga kilichopo jijini Dar es Salaam,” amesema Kitiku

Akizungumza wakati akichangia hoja hiyo, Waziri Simbachawene amewataka Jeshi la Magereza pindi mradi huo utakapoanza watengeneze mkate bora wakizingatia suala nzima la masoko, teknolojia bora ikiwapo ladha ya mkate huo, vifungashio vyake ili waweze kwenda sambamba na hitajio la mtumiaji wa mwisho

“Ni wazo zuri kwa mlichopanga kwani mtakapofanikiwa mtakua mmeongeza kipato na ile dhana ya jeshi la magereza kujitegemea itakua sasa imeingia kwenye utekelezaji sambamba na kujitosheleza kwa chakula cha kulisha wafungwa,” amesema

“Lakini katika mpango huo lazima baadhi ya mambo muyafanyie utafiti ikiwapo soko linataka nini, teknolojia mtakayotumia muhakikishe ni nzuri itakayowafanya mpate bidhaa yenye ladha nzuri sambamba na kifungashio cha bidhaa hiyo, ni vizuri mmeliweka wazo wazi mapema nadhani mtapata michango ya kuliboresha,” amesema Waziri Simbachawene

Jeshi la Magereza limeomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh201.25 bilioni  katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwamo miradi ya maendeleo huku likiweka lengo la kukusanya maduhuli ya Sh2 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.