Jinsi Katibu Mkuu CUF alivyotabiri kifo chake

Ilikuwa kama nadhiri kwa Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa ambaye kwenye mikutano yake mingi alinukuliwa akisema ‘atafia CUF’. Na ndivyo ilivyokuwa kifo kimemkuta ndani ya chama hicho licha ya misukosuko mingi zikiwamo kesi mahakamani.

Nadhiri hiyo ilikuwa ya Khalifa ambaye alifariki dunia Machi 30, 2020, hospitalini wakati akipatiwa matibabu na alizikwa makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Pengine unaweza kusema nadhiri ya Khalifa ilitokana na yeye kuwa miongoni mwa waasisi wa CUF. Inaelezwa kipindi hicho Khalifa alikuwa mwalimu wa sekondari ambaye aliamua kuacha kazi hiyo ili kupigania haki.

Licha ya kusema atafia CUF, pia aliwahi kunukuliwa akisema chama hicho hakiwezi kufa kwa sasa kutokana na uongozi mpya ambao umeingia madarakani ukiongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba.

Kauli ya CUF haitakufa aliitoa baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na wafuasi wengine wa chama hicho kuhamia ACT- Wazalendo.

“Alikuwa mtu mwenye msimamo kwani hata baada ya chama cha CUF kupata misukosuko na kupasuka pande mbili yeye alibaki na msimamo wake. Hakuwa na siasa za kumfuata mtu.

“Alishutumiwa kwa kuitwa msaliti pale alipomuunga mkono Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba, alituhumiwa kuhusu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa sababu ya urafiki wao, mara aliambiwa yeye ni pandikizi wa CCM.

“Lakini alibaki na msimamo wake kwamba atafia CUF, na kweli Mwenyezi Mungu amemsikia na amekufa akiwa Katibu Mkuu wa CUF,” anasema Ahmed Juma Ngwali ambaye mwezi uliopita alijiondoa CUF na kujiunga na CCM.

Anasema Khalifa alikuwa mvumilivu na mwenye utu na kuna wakati ndani ya Bunge aliwashutumu wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi ambao waliamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakisusa muswada wa mabadiliko ya Katiba na ndio ulikuwa mwanzo wa mchakato wa Katiba mpya. Ngwali anasema Khalifa alikuwa nguzo kwenye chama cha CUF na kwamba pengo lake litakuwa gumu kuliziba na huenda ikachukua muda mrefu.

Anasema Khalifa alianza kupigania haki, wakati huo Tanzania ilikuwa bado haijaruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini tayari harakati za kudai mfumo wa vyama vingi zilikuwa zimekwisha anza.

Kikwete atuma salamu

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alituma salamu kupitia ukurasa wake wa Twitter na kusema “Ni kweli tulikuwa pande mbili tofauti lakini kama wanadamu tulikuwa marafiki tangu wakati tukiwa wote Bungeni na hata baada ya Mimi kuacha Ubunge. Daima nitamkumbuka kwa moyo wake wa upendo, ukarimu, ucheshi na huruma. Tuko pamoja katika majonzi na kuomboleza.”

Msimamo wa kisiasa

Wakati CUF inaingia katika mgogoro wa uongozi na kusababisha hata wabunge kugawanyika, Khalifa hakuyumba licha ya kwamba anatoka kisiwani Pemba ambako ni ngome ya Maalim Seif.

Hata wakati baadhi ya wanachama wakimfuata Maalim Seif alipohamia ACT- Wazalendo, bado aliendelea na msimamo wake wa kutofuata mtu na hatimaye akachaguliwa kuwa katibu mkuu.

Aliamini katika kusimamia taratibu, kanuni, sheria na katiba ya chama badala ya kuwa bendera fuata upepo licha ya kwamba anatoka kisiwa kimoja na Maalim na huenda hali hiyo ilisababisha wakawa mahasimu.

Msimamo wake haukuwa kwenye hilo tu bali hata mambo yanayohusu maslahi ya Zanzibar, alikuwa mstari wa mbele kuyatetea bungeni bila woga wala kigugumizi hadi kukwaruzana na wabunge wenzake.

Iliwahi kutokea kutaka kukunjana na mbunge mmoja nje ya ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, baada ya mbunge huyo kuwarushia ‘madongo’ wabunge kutoka visiwani Zanzibar wakati wakijadili maslahi ya muungano.

Pamoja na hayo, Khalifa alikuwa ni mtu anayependa msamaha, kwani hata baada ya kuibuka na ushindi na kuukwaa ukatibu mkuu wa CUF aliwataka wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kusameheana.

Wakati wa uhai wake alikaririwa na vyombo vya habari akiwaambia wajumbe kuwa chama kimeshapata uongozi mpya, na sasa wanachama kusameheana na kujenga umoja mpya kwa maendeleo ya chama.

Kwamba CUF kimepita katika mikwaruzo mingi, hivyo wanachama wanatakiwa kuweka ubinadamu mbele kwa kuachana na yaliyopita kwa sababu hayajengi.

Aliweka wazi kuwa wanachama walioondolewa uanachama wao na mkutano mkuu siwezi kuzungumza lolote kwa sababu huo ni uamuzi wa wajumbe wa mkutano mkuu, lakini wengine waliobaki wasameheane.

“Watusamehe na sisi tuwasamehe kwa sababu tumepita kwenye mikwaruzano mikubwa, tumeshambuliana vya kutosha, tumesemana vya kutosha na mimi kwa nafasi yangu napenda kuwaambia wanachama kwamba yaliyopita si ndwele tugange yajayo kwa maendeleo ya CUF yetu,” alihimiza Khalifa enzi ya uhai wake.

Baada ya hapo, Khalifa alianza kazi za chama na kufika katika ofisi zake jijini Dar es Salaam na kukuta zimefungwa kwa muda, lakini akasema pamoja na hali hiyo ataendelea na majukumu yake kama kawaida.

Mwanzo wa CUF

Zanzibar kulikuwa na kikundi kilichojiita Kamahuru kikipigania demokrasia kwenye visiwa vya Unguja na Pemba. Na Bara kulikuwa na kikundi cha kupigania haki za binadamu Tanzania Bara kilichoitwa Civic Movement.

Mei 28, 1992 vikundi hivyo viwili Kamahuru na Civic Movememnt viliungana na kuzaliwa chama cha The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi).

Katika historia hiyo huwezi kumuweka pembeni Khalifa ambaye katika jimbo lake la Gando kisiwani Pemba alikuwa wa kutiliwa mfano katika kupigania siasa zenye haki.

Ngwali anamuelezea Khalifa kwamba alikuwa ni mfano wa kuigwa kwenye siasa za Pemba na kwamba hata yeye ndiye aliyemfanya aingie kwenye siasa hadi kuwa mbunge. Machi 2, 2020 Ngwali alijivua uanachama wa CUF na kuhamia CCM.

Ngwali anamtaja Khalifa kama baba yake kiumri, lakini pia ni mwalimu wake katika siasa na maisha ya kawaida katika jamii.

Anamtaja Khalifa kama mwalimu wake kwa kuwa alikuwa akivutiwa na hotuba zake kwenye mikutano ya kisiasa kwa namna alivyojali matatizo ya jamii.

Pia, anamtaja Khalifa kama mwalimu wake katika siasa za kimataifa kwa namna alivyokuwa mtetezi mzuri wa masilahi ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje.

“Unajua Khalifa kijijini kwake alikuwa akitegemewa sana kutokana na busara na uvumilivu aliokuwa nao katika jamii, aliwasikiliza watu na aliwasaidia pale alipokuwa na uwezo,” anasema Ngwali.

Michango yake kisiasa

Khalifa mbali na ubunge amekuwa mzungumzaji mzuri katika majukwaa ya kisiasa katika kudai haki kwa ajili ya wananchi alipokuwa kwenye nafasi ya ubunge alikuwa na mchango mkubwa bungeni na moja ya michango yake ni huu.

Mfano aliwahi kunukuliwa akisema; Kwanza tukwambie baadhi ya mambo yanayotekelezwa ndiyo ulikuwa msimamo wa chama chetu. Mfano, wananchi kunufaika na rasilimali za nchi yao kama vile madini na vitu vingine, hiyo ni sera ya chama chetu.

Kwa vile anaitekeleza Rais wa nchi, sisi kwetu ni fahari, tunahisi anafanya kile ambacho tulidhamiria kuwafanyia wananchi kama tungepata ridhaa ya kuongoza nchi.

Na huwezi kufumba macho mbele ya maendeleo, kuna mambo mengi makubwa anayafanya, kwa mfano la rushwa limepungua kwa kiwango fulani, matumizi mabaya ya fedha za umma yamepungua kwa kiasi fulani, ingawa tuna tatizo bado, maana watu wa kawaida wangali wana dhiki, hawapati mkate, hawawezi kujua haya ni maendeleo.

Lakini, sisi watu ambao ni viongozi wa vyama, ambao tupo katika nchi yetu kwa muda mrefu, tunahisi Rais (John) Magufuli anafanya mambo makubwa.

Kwa hiyo nitumie fursa hii nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhudumia Watanzania, lakini nimwambie wakati umefika sasa wa kuiachia demokrasia ichukue mkondo wake, suala la kubana kwenye mikutano ya hadhara ajue haki ya demokrasia katika nchi imepitishwa kisheria, ipo kwenye katiba. Yeye na chama chake hawawezi wakafanya siasa, sisi wakatuzuia tusifanye, hiyo si haki.