Jinsi Nyerere alivyoomba kura 1975, Aboud Jumbe atetea urais Zanzibar

Thursday March 26 2020

 

By William Shao, Mwananchi

Usiku wa Oktoba 24, 1975, siku mbili kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 26, Rais wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere alilihutubia Taifa kwa njia ya redio na kuahidi kuwa ataendelea kuitumikia Tanzania na watu wake kwa kipindi kingine cha miaka mitano kama wananchi wengi wangempigia kura.

Na kwa upande wa Zanzibar, Aboud Jumbe ambaye aliingia madarakani Aprili 1972 baada ya kifo cha Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kilichotokea Aprili 7, 1972, uchaguzi huu ulikuwa wa kwanza kwake na ndiyo uliomuweka madarakani.

Katika hotuba yake, Nyerere alisema kwa mara ya nne Tanzania Bara na mara ya tatu katika Zanzibar, vyama vya Tanu na Afro-Shirazi vimempa heshima kwa kupendekeza jina lake ili lithibitishwe kuwa ndilo jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kama mtakubali pendekezo hilo na mtakubali. Ikiwa wengi zaidi kati ya wapigakura watasema “Ndiyo” katika karatasi ya uchaguzi, basi nitaendelea kuitumikia nchi yangu na wananchi wenzangu kwa kipindi kingine cha miaka mitano,” alisema.

“Lakini mimi naweza kutamka tu kwamba niko tayari tena kutumikia nchi yangu na wananchi wenzangu, lakini wanaomchagua Rais ni ninyi.”

Mwalimu Nyerere ambaye alianza hotuba yake kwa kuelezea umuhimu wa kuchagua viongozi wanaofaa na wenye uwezo kama ilivyokuwa katika Ilani ya Uchaguzi, alitoa rai kwa watu wote waliojiandikisha, kufika vituoni na kupiga kura.

Advertisement

Siku moja kabla ya kupiga kura, makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Pius Msekwa alisema katika matangazo ya redio, wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze kwa wingi.

Msekwa alisema matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yangetangazwa rasmi Ijumaa, Oktoba 31 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Siku ya kupiga kura, yaani mamilioni ya watu walijitokeza kupiga kura kote nchini. Wakati Tanzania Bara wakichagua Rais, wabunge na madiwani, Zanzibar walimchagua Rais peke yake.

Kazi hiyo ya kupiga kura ilikamilika mapema alasiri.

Hata hivyo, wapigakura waliofika mapema asubuhi vituoni walilalamika kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa vifaa na kuwafanya wasubiri kwa muda mrefu.

Mwalimu Nyerere alikuwa miongoni mwa wananchi waliopiga kura zao kituo cha Shule ya Msingi Msasani.

Baada ya kupiga kura, alitembelea baadhi ya vituo vya wilayani Temeke, Ilala na Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Kibaha Mkoani Pwani.

Huko Visiwani Unguja na Pemba, Makamu wa Kwanza wa Rais, Jumbe alikuwa miongoni mwa maelfu ya wapigakura.

Baada ya kupiga kura yake, alivitembelea vituo mbalimbali vya uchaguzi mjini Zanzibar.

Matokeo kwa upande wa wabunge yalianza kumiminika Oktoba 27 katika Ofisi za Bunge mjini Dar es Salaam kutoka majimbo mbalimbali ya uchaguzi.

Matokeo ya awali yalionyesha mawaziri waliokuwa wameshinda kuwa ni Amir Jamal wa jimbo la Morogoro Mjini aliyepata kura 12,783 wakati mpinzani wake, Kingalu Ramadhani Kingalu, alipata kura 2,208. Kura 360 ziliharibika.

Daudi Mwakawago aliyegombea jimbo la Iringa Mjini alipata ushindi wa kura 10,325 na mpinzani wake, Hudi Mbarazi (2,538). Kura 347 ziliharibika.

Katika jimbo la Songea Mjini, Gisler Mapunda alishinda kwa kura 9,627 wakati mpinzani wake, Oswald Komba alipata kura 1,176 na kura 280 ziliharibika.

Jimbo la Tanga, Omari Muhaji alishinda kwa kura 23,653 huku mpinzani wake, Abdallah Liku akipata kura 10,506. Kura 96 ziliharibika na karatasi 505 hazikuwa na alama yoyote.

Huko Tabora Mjini, Paulo Misingalo alishinda kwa kupata kura 10,635.

Alimshinda Saleh Tambwe ambaye alikuwa Waziri Mdogo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyepata kura 8,950. Kura zilizoharibika zilikuwa 448.

Moshi Mjini, Muhidini Kimario alishinda kwa kura 16,705 dhidi ya mpinzani wake, Lucy Lameck ambaye alikuwa mbunge wa siku nyingi, aliyepata kura 2,234. Kura 553 ziliharibika.

Katika jimbo la Kahama, Luis Sazia alipata kura 30,015 na Mwanamahega Fares (4,414), Jimbo la Mwanza mshindi alikuwa Daniel Machemba (kura 28,491) dhidi ya Samuel Malundi (11,595) na Mtwara Vijijini, alishinda Yusuf Hamis Nabalang’anya (46,170) dhidi ya Hassani Mbaula (5,674).

Matokeo mengine yaliyopatikana mchana wa Oktoba 27, 1975 yalikuwa ya Jimbo la Arusha ambako Solomoni Ole Saibul alipata kura 20,110 dhidi ya Halima Maliyakora (6,224). Kura zilizoharibika zilikuwa 475.

Wilayani Chunya, Felix Mwanambilimbi alipata kura 13,812 na kumshinda Edward Mwangasini Kalupale (9,094), na Jimbo la Mafia alishinda Ayubu Kimbau (5,667) dhidi ya Mwinyimzee Kijombe (2,015).

Katika jimbo la Mtwara Mjini, Khalida Zalari alishinda kwa kupata kura 10,171 na kumshinda Mohamed Chereheni aliyepata kura 5,995. Kura 812 ziliharibika.

Wilayani Pangani, Tobi Mweri alipata kura 8,626 wakati Fadhili Bwanga akipata kura 1,578 na zilizoharibika zilikuwa 237.

Jimbo la Korogwe lilichukuliwa na Hussein Shekilango aliyepata kura 34,845 dhidi ya kura 14,224 za Athumani Mhina.

Katika jimbo la Shinyanga Vijijini, mshindi alikuwa Edward Nzigula aliyepata kura 41,608 dhidi ya Philipo Kiariro aliyepata kura 26,688. Kura zilizoharibika zilikuwa 397.

Mkoani Pwani, Adrian Mapande alishinda Jimbo la Bagamoyo kwa kura 25,116 dhidi ya Stephen Semindo aliyepata kura 10,508. Zilizoharibika ni 227.

Jimbo la Manyoni mshindi alikuwa Margareth Ndaga kwa kupata kura 13,335 wakati mpinzani wake, Simon Mwaluko alipata kura 12,458. Kura zilizoharibika zilikuwa 156.

Jimbo la Ilala mshindi alikuwa Kitwana Kondo aliyepata kura 60,241 na kumshinda mpinzani wake, Martha Weja aliyepata kura 14,400. Zilizoharibika zilikuwa kura 1,660.

Jimbo la Shinyanga Mjini aliyeshinda alikuwa Frederick Fumbuka aliyepata kura 9,278 na kumshinda mpinzani wake, Joseph Kabodo aliyepata kura 6,021. Kura zilizoharibika ni 253.

Bariadi aliyeshinda ni Edward Masanya aliyepata kura 39,856 dhidi ya kura 7,971 za mpinzani wake, Masuke Tunge na zilizoharibika zilikuwa ni kura 184.

Jimbo la Kinondoni mshindi alikuwa Derek Byceson aliyepata kura 88,572 na kumshinda Mary Chipps aliyepata kura 20,151. Kura zilizoharibika zilikuwa 1,001.

Hayo ni matokeo ya baadhi ya majimbo. Matokeo ya urais yalikuwa ya mwisho kutangazwa.

Katika uchaguzi huo, vijana 31 walifanikiwa kuingia bungeni. Vijana hao walikuwa na umri kati ya miaka 31 na 40.

Pia kulikuwa na idadi ndogo ya wabunge wenye umri chini ya miaka 30. Wabunge hao walioanzia miaka 21 hadi 30 walikuwa wanne, sawa na idadi ya wazee waliozidi umri wa miaka 61.

Wazee, wenye umri wa kati ya miaka 51 na 60 walikuwa 14.

Pia kulikuwa na wabunge wanawake 16.

Uchaguzi wa mwaka 1975 ulikuwa wa tatu uliohusisha chama kimoja baada ya mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1965, ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi.

Awali Tanzania iliendesha chaguzi zake kwa kutumia mfumo wa vyama vingi, lakini mabadiliko hayo ya 1975 yaliingiza nchi katika siasa za chama kimoja hadi mwaka 1992 wakati nchi ilipolazimika kufuata wimbi la mageuzi ya kisiasa lililotanda duniani kote.

Kesho tutawasoma vigogo walioshinda na walioangushwa katika uchaguzi huo.

Advertisement