Breaking News

Jinsi S2keezy alivyovamiwa studio

Friday October 16 2020

By Kelvin Kagambo

Dar es Salaam. Jana Oktoba 15, 2020 mitandao ya kijamii iliamshwa na habari ya uvamizi uliofanywa kwenye studio za muziki za Pluto Nation zilizopo Sinza Dar es Salaam zinazomilikiwa na prodyuza S2keezy.

Kupitia akaunti yake ya Instagram S2keezy aliandika kuwa watu waliojitambulisha kuwa ni askari wa sungusungu walivamia studio hizo zilizopo Sinza Dar es Salaam na kufanya uhalifu ikiwemo kuvunja vitu vya studio pamoja na kuwapiga na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji watu waliokuwepo studio humo.

Tovuti ya Mwananchi ilimtafuta S2keezy na kuzungumza naye kwa njia ya simu ambapo ameeleza stori kamili ya tukio lilivyokuwa.

Ilikuwa hivi; S2keezy ameeleza, yeye na wenzake walikuwa na kazi ya kwenda ‘kushot’ video ya muziki alfajiri ya Oktoba 15, kwa hiyo ili kurahisisha kazi walikubaliana wakutane hapo studio ili watoke kwenda pamoja.

“Kwahiyo wote tulikuwa hapa (studio). Mimi ilipofika muda nikatoka kwenda kufata usafiri pamoja na kufuata gari yangu kwa sababu niliiacha kwa Felix (rafiki yangu). Niliporudi ndo nikakuta hii hali.” ameeleza.

Amesema alikuta mlango umevunjwa, alipoingia ndani pia akakuta vitu vimerugika, mfano baadhi ya spika, kompyuta na TV vilikuwa chini vimetupwa.

Advertisement

“Pia ,wenzangu walikuwa wamepigwa, wamejerehiwa. Na sio kupigwa tu hata walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji, kwa mfano waliambiwa wavue nguo, na tena kulikuwa na wanawake na wanaume sehemu moja,” ameeleza S2keezy.

Serikali, viongozi waingilia kati baada ya tukio hilo Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas alifika katika studio hizo kwa ajili ya kuwatazama na kuwapa pole waathirika wa tukio hilo ambao ni wasanii mbalimbali wengi wakiwa chipukizi, akiwamo Hanstone aliyeimba wimbo wa Iokote na Maua Sama.

Akizungumza na wasanii Dk Abbas amesema Serikali inatambua na kuheshimu sanaa inayofanywa na amewaahidi watashuhulikia jambo hilo kwa sababu limeshafikishwa mahala husika, chini ya Jeshi la Polisi.

“Serikali inatambua na kuziheshimu shughuli za sanaa, Kwahiyo tumesikia hili tukio, na nafahamu kuna kesi polisi kwa maana ya hao Sungusungu waliokuja hapa wanadai walikuja kuzuia tukio fulani na ninyi, hawa (wasanii) wanasema walivamiwa, kwahiyo hii ni kesi ya kipolisi zaidi,” amesema Dk Abbas.

Pia, Katibu wa Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter akiwapa pole walioathirika na tukio hilo kueleza imani yake juu vyombo vya dola vitakavyotenda haki juu ya hilo.

Taarifa zaidi endelea zijakuja

Advertisement