Jinsi corona ilivyobadili utaratibu vikao vya Bunge

Spika wa Bunge Job Ndugai, akizungumza wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na Mkutano wa 19 wa Bunge la 11 unaotarajia kuanza kesho bungeni jijini Dodoma. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mkutano wa Bunge unaanza kesho Jumanne Machi 31, 2020 mjini Dodoma  huku uendeshaji wa chombo hicho cha Dola ukibadilika kwa kiasi kikubwa lengo likiwa ni kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona

Dodoma. Mkutano wa Bunge unaanza kesho Jumanne Machi 31, 2020 mjini Dodoma  huku uendeshaji wa chombo hicho cha Dola ukibadilika kwa kiasi kikubwa lengo likiwa ni kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 30, 2020 Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema vikao vya mkutano huo wa 19 Bunge la 11 vitaanza kesho na kumalizika Juni 30, 2020  lakini kutakuwa na mabadiliko ikiwemo la kikao kuanza saa 8 mchana na kumalizika saa 12 jioni, badala ya kuanza saa 3 asubuhi na kumalizika saa 1:30 jioni.

Amesema katika mikutano mingine walikuwa wakikutana kwa saa 9 ama zaidi lakini katika mkutano huo watakutana kwa saa zisizozidi nne.

 

Amesema nyaraka zote kutoka serikalini  zitawafikia wabunge na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao.

 

Amesema kesho kikao kitaanza saa 3 asubuhi kwa sababu Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akiahirisha mkutano wa 18 wa Bunge alisema kuwa anaahirisha hadi saa 3:00 asubuhi.

 

“Kuanzia keshokutwa tutaanza saa 8 mchana..., kwa hiyo ndani ya Bunge kutakuwa na wabunge wasiozidi 150 kwa wakati kutoka ile namba niliyosema ya zaidi ya watu 700,” amesema.

 

Amesema mawaziri wote watazungumza kutoka alipokaa kwa kutumia kipaza sauti na si kwenda mbele kwenye mimbari kama ilivyozoeleka.

 

“Hakutakuwa na maswali na majibu kama ilivyozoeleka. Yote  yataingizwa katika mtandao wa tablet za wabunge asubuhi ya siku husika. Na kama mbunge ana maswali ya nyongeza ataandika na swali litaingia katika mfumo wetu wa Bunge,” amesema.

 

Amesema mawaziri watapata maswali hayo na  kabla ya saa 7:00 mchana yatakuwa yamewafikia wabunge.

 

Amesema hakutakuwa na maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu katika mkutano wote wa Bunge.

 

Amesema wabunge wengine ambao hawataingia katika ukumbi wa Bunge, wataingia katika kumbi nyingine zilizoandaliwa na watafuatilia vikao vya Bunge kwa njia ya video.

 

Ndugai amesema wataweka utaratibu ambao kila mbunge ataweza kupiga kura bajeti ya mwaka 2020/21 kupitia tablet yake.

Amesema siku ya kupitisha bajeti kuu kikatiba kila mbunge anatakiwa kupiga kura, hivyo wataweka utaratibu ambao wabunge wataingia kwa awamu kwa ajili ya kupiga kura.