Jinsi kutojiamini kunavyowakwamisha wanawake

Muktasari:

Waziri wa Elimu nchini Tanzania,  Profesa Joyce Ndalichako amesema kutokujiamini ni moja ya jambo linalowafanya wanawake kushindwa kufanya uamuzi, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu nchini Tanzania,  Profesa Joyce Ndalichako amesema kutokujiamini ni moja ya jambo linalowafanya wanawake kushindwa kufanya uamuzi, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua semina ya siku saba iliyowakutanisha wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30 kutoka nchi 17 duniani.

Semina hiyo inayolenga kuimarisha ushiriki wao katika masuala ya jinsia, utamaduni na uongozi imeandaliwa na taasisi isiyo ya serikali ya Tanzania Girls Guide Association (TGGA).

Katika maelezo yake Profesa Ndalichako  amesema baada ya  semina hiyo wasichana watakuwa na uwezo wa kukemea imani potofu kuwa wanawake ni viumbe dhaifu.

“Itawafanya wawe na uamuzi wa msingi, wataendelea kutengeneza mtazamo chanya kuwa wanawake wanaweza kuleta matokeo chanya kama wenzao wanaume kwa sababu wengine licha ya kuwa na uwezo wanakosa kujiamini.”

“Lakini si tu kushiriki katika vikao vya maamuzi ya kijamii lakini pia tunataka washiriki vikao vya maamuzi ya kutengeneza sera,” amesema Profesa Ndalichako.

Ameongeza, “nchi yetu imepiga hatua katika kuonyesha usawa wa kijinsia na hii ni baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kumchagua makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mwanamke.”

Mwenyekiti wa bodi ya TGGA, Anna Maembe amesema mbali na siku saba za kujifunza mambo mbalimbali pia washiriki wa semina hiyo watashiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea shule za watoto yatima na kushiriki masuala ya utamaduni.