Jinsi wahitimu mafunzo benki walivyowasaidia viziwi

Muktasari:

Benki ya GT Tanzania imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia, michezo na malazi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Buguruni Viziwi iliyopo jijini hapa.

Dar es Salaam. Benki ya GT Tanzania imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia, michezo na malazi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Buguruni Viziwi iliyopo jijini hapa.

Msaada huo wa  zaidi ya Sh4 milioni umetolewa na wahitimu wa mafunzo kwa vitendo wa  benki hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, mkurugenzi wa benki hiyo, Jubril Adenji amesema msaada huo ni kati ya vitu wanavyofundishwa katika benki hiyo, “kama benki tumekuwa na utaratibu wa kuchukua vijana wanaohitimu masomo yao kutoka vyuo mbalimbali na kuwapatia mafunzo ya kazi kwa miezi mitatu.”

“Mbali na kuwafundisha kuhusu utendaji kazi tumekuwa tukiwafundisha kumudu maisha na kuwasisitiza umuhimu wa kurudisha kwa jamii kwa sababu tunaamini jamii tunayoihudumia ni lazima tuirudishie,” amesema Adenji

Mjumbe wa bodi wa benki hiyo, Francis Nanai aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanikiwa katika malengo waliyojiwekea.

“Watoto wana haki ya kupendwa, kusikilizwa na kupewa malezi na makuzi mazuri ndio maana Serikali na wazazi wamewaleta hapa mnafundishwa vizuri ikiwemo heshima, tunawaomba mtumie fursa hiyo kusoma vizuri na kwa bidii,” amesema Nanai

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Richard Kweka alishukuru msaada walioupata kutoka kwa benki hiyo huku akiomba kupatiwa msaada wa vifaa zaidi kwa ajili ya kujifunzia.

“Baada ya kupata ujuzi tunatamani wanafunzi hawa waendelee kusaidiwa kutengeneza bidhaa zinazouzika kwa watu,” amesema.

Baadhi ya msaada waliopewa ni unga, mchele, vifaa vya usafi ikiwemo fagio, kwanja, leki, taulo za kike.