Jinsi wanandoa raia wa China walivyodakwa wakimpa Sh11 milioni bosi TRA wasamehewe kodi

Wednesday February 26 2020

Watuhumiwa wanao daiwa kutoa rushwa kwa

Watuhumiwa wanao daiwa kutoa rushwa kwa kamishna wa TRA  Zeng Ronglan  (kushoto) ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Ronglan  ITL  INTL  kushoto mwanaume akiwa na mwezake  OU YA kulia wote ni wakazi wa Mafinga Iringa wakitoka katika mahakama ya hakim mkazi kisutu kusomewa shitaka lao la Rushwa Picha na  Omar Fungo       

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ipyana Mwakatobe ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi Zheng Rongman (50) na mkewe Ou Ya (47) walivyompa rushwa ya Sh11.5 milioni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Dk Edwin Mhede ili wasamehewe kodi.

Ameeleza hayo leo Jumatano Februari 26, 2020 katika mahakama hiyo wakati akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambao wamekiri makosa na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja.

Rongman ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ronglan Intl Industry and Trade Co. Ltd na mkewe ni raia wa China na wakazi wa Kinyanambo, wilaya ya Mafinga mkoani Iringa.

Mbali na kulipa faini, mahakama hiyo imetaifisha Sh11.5milioni kuwa mali ya Serikali.

Hadi leo saa 6:30 mchana walikuwa hawajalipa faini na kurudishwa mahabusu.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakamani hiyo, Huruma Shaidi amesema washtakiwa wametiwa hatiani baada ya kukiri kosa lao la kutoa rushwa.

Advertisement

"Washtakiwa mmetiwa hatiani kama mlivyoshtakiwa mahakama inawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh1 milioni na pia kiasi cha Dola za kimarekani 5,000 ambacho ni sawa na Sh11.5milioni mlizotaka kumpa kamishna mkuu wa TRA, zinataifishwa na kuwa mali ya Serikali.”

“Hata kama ni mwekezaji unatakiwa kufuata sheria, wawekezaji wote  wanatakiwa wafuata sheria na taratibu zilizopo hapa nchini, haipendezi mwekezaji akavunja sheria za nchi,” alisema Hakimu Simba.

Hakimu Shaidi amesema washtakiwa hao mara baada ya kulipa faini hiyo, wapelekwe  makao makuu ya TRA ili kwenda kulipa kodi wanayodaiwa.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu, wakili wa utetezi, Steven Bwana akisaidiana na Peter Lyimo na Denis Mdoe, aliomba Mahakama iwapunguzie adhabu.

Bwana amedai washtakiwa hao ni kosa lao la kwanza na kupitia kampuni yao, wameweza kutoa ajira kwa watanzania 100 na wana familia inayowategemea.

Awali, Mwakatobe amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao( PH).

Amedai Februari 24, 2020 washtakiwa hao walifika makao makuu TRA Wilaya ya Ilala kwa ajili ya kuonana na Dk Mhede.

Mwakatobe amedai siku ya tukio saa 10:00 jioni washtakiwa hao walionana na bosi huyo wa TRA ofisini kwake akiwa na msaidizi wake, walimueleza kuwa wana tatizo na kodi na waliwasilisha nyaraka kadhaa wakidai  wamekadiriwa kiwango kikubwa cha kodi, kumuomba kamishna huyo atatue mgogoro huo.

Baada ya kueleza hayo walitoa burungutu la fedha ambazo ni Dola 5,000 za Kimarekani na kumkabidhi kamishna huyo, kama kishawishi ili aweze kuwasaidia katika suala lao la kodi. Kampuni hiyo ilipaswa kulipa kodi ya Sh1.3 bilioni.

Mwakatobe amedai Dk Mhede alimuelekeza msaidizi wake kuzihesabu fedha hizo alizopewa na washtakiwa na kubaini zilikuwa Dola 5,000 za Kimarekani.

Amesema kamishna huyo baada ya kuona hali hiyo,  alitoa taarifa Takukuru na maofisa wa taasisi hiyo walifika TRA kuwakamata washtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa

Advertisement