Juma Nature atoboa siri ya bifu la Diamond, Ali Kiba

Thursday October 31 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwanamuziki Juma Nature amezungumzia kitendo cha Ali Kiba kumjibu Diamond Platnumz  aliyemualika kushiriki tamasha la Wasafi akisema kinachowaponza wawili hao ni mashabiki.

“Watengeneze msingi ulio bora kwani baada ya wao kuwa juu kwa sasa kuna muda wasanii wengine watakuja na kuwa juu kama walivyo wao hivi sasa, watumie muda wao vizuri,” amesema Juma Nature, mmoja kati ya wasanii waliokuwa wanaunda kundi la muziki wa kizazi kipya la TMK wanaume Family lililojizolea umaarufu kabla ya kuvunjika mwaka 2006.

Juma Nature ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 baada ya kuulizwa na Mwananchi kilichoibuka jana kati ya wasanii hao.

Jana asubuhi, Diamond aliulizwa swali katika mkutano wake na waandishi wa habari kama Ali Kiba na Harmonize watashiriki katika tamasha la Wasafi ambalo ametangaza kuwa litafanyika Novemba 9, 2019.

Nyota huyo wa kibao kilichotikisa Afrika cha “Number One” alijibu kuwa ameuandikia uongozi wa Ali Kiba kuomba ushiriki wa mtunzi huyo wa wimbo maarufu wa “Aje”. Pia Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nassib Abdul, alisema hakuna haja ya kuendeleza “bifu (mzozo) ambao hakuutaja, baina yake na Ali Kiba.

Lakini kauli yake kwa waandishi wa habari haikumfurahisha Ali Kiba na katika akaunti ya mtandao wa kijamii ya officialalikiba, alitoa maneno makali bila ya kumtaja anayemshambulia.

Advertisement

“Usiniletee mambo ya darasa la pili, unaniibia penseli halafu unan-isaidia kutafuta,” ameandika bosi huyo wa Kings Record Label.

“(UNIKOME). Mwanaume huwa anaongeaga mara moja tu, sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu. Sasa tuishie hapo, nakutakia tamasha jema.”

Juu ya ujumbe huo kuna picha ya Ali Kiba akiwa amekaa kwenye kiti, amevalia suruali aina ya jeans na shati la mikono mirefu bila ya kufunga vifungo.

Kiti hicho kiko pembeni ya kabati la vitabu na sehemu ya kati kuna pembe ya ng’ombe iliyopakwa rangi nyekundu, njano na nyeusi, ikiwa katikati ya vitabu vichache vilivyosimamishwa na mwanzoni mwa kila upande kuna mtungi wenye rangi hizo.

“Kwa ushauri wangu Ali Kiba angekubali kuhudhuria shoo hiyo kwani kikubwa ni kupata fedha na kuweka tofauti zao pembeni bila kujali watu watasema nini.”

"Kama ni kugombana wao sio wa kwanza, watu waligombana na wake zao na wakapatana sembuse wao, katika hili waangalie pia suala la maendeleo, kwani watakapopata fedha katika shoo hiyo zitawasaidia kufanya mambo yao yasonge mbele,” amesema Juma Nature.

Amesema ndiyo maana TMK Wanaume licha ya kutengana kwa muda mrefu linapokuja suala la fedha huweka tofauti zao pembeni na kufanya kazi.

 “Mimi ninachoangalia ni fedha na maendeleo ukifanya shoo ukalipwa kuna watu wengi wananufaika nyuma yako, sisi tutaungana na tutapiga shoo ya maana kwenye tamasha la Wasafi, ”amesema Nature.

 

 

Advertisement