KKKT yatoa maagizo kudhibiti corona, ibada sasa ni dakika 45 tu

Moshi. Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imetoa maagizo kadhha kwa waumini wake ikiwamo kutaka ibada zifanyike kwa dakika 45 tu badala ya saa moja na nusu.

Lengo la maagizo hayo ni kukabiliana na maambukizi ya Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Ugonjwa huo uliosambaa katika nchi mbalimbali duniani, Tanzania ina watu 20 waliothibitika kupata maambukizi, watatu wamepona na mmoja amefariki.

Katika maagizo ya KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, ibada zote sasa zitakuwa fupi zisizozidi dakika 45 badala ya saa moja na nusu na Wakristo wametakiwa kukaa tofauti ya umbali wa mita moja au mbili.

Andiko la maagizo hayo ambalo litasomwa makanisani katika sharika zote za dayosisi hiyo kuanzia leo, limetiwa saini na Askofu wa dayosisi hiyo, Fredrick Shoo na katibu mkuu wake, Arthur Shoo.

“Hayo ni maagizo ya Halmashauri Kuu ya Dayosisi yetu na yatasambazwa kwenye sharika zetu zote,” alisema Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa KKKT.

Kwa mujibu wa andiko hilo mbali na kutaka ibada ziwe fupi, pia zimetakiwa kuwa mbili hadi tatu ili kupunguza msongamano na pia wataalamu wa afya waalikwe kutoa elimu kwa washarika.

“Ibada ya nyumba kwa nyumba iwe kwa familia tatu mpaka nne na idadi ya watu isizidi 20. Ibada hizi zifanyike nje na pia viti viwe na umbali wa kati ya mita moja na mbili,” linaelekeza andiko hilo.

Kanisa hilo limewataka wazee wa miaka 70 na kuendelea na wenye magonjwa sugu wapate ushauri kwanza kwa wataalamu wa afya kuhusu kuhudhuria ibada hizo.

Pia Halmashauri Kuu imewaelekeza washarika watakaoshindwa kwenda kanisani kwa sababu ya ugonjwa, wanaweza kutuma sadaka zao kupitia miamala ya simu kama M-Pesa na Tigo Pesa.

“Kabla na baada ya ibada viti, meza pamoja na vipaza sauti visafishwe kwa dawa na ibada za mazishi ziwe na watu wachache wa familia moja na majirani,” imesisitiza malmashauri kuu.

“Ibada za send-off na harusi zihusishe watu wachache wa karibu na familia husika na pia mazingira yaandaliwe kwa kufuata kanuni za afya. Tunashauri pasiwepo na sherehe,” linaeleza andiko hilo.

Pia Dayosisi hiyo imeviagiza vituo vya afya vilivyopo chini ya dayosisi hiyo, kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na watumishi wa kada isiyo ya afya wachukue likizo.

Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki (TEC) nalo tayari limeshatoa mwongozo wa ibada, likiwataka waumini kuzingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi ikiwamo kunawa mikono na sabuni.

Tamko la TEC la Machi 26 ,2020 lilisainiwa na Rais wa Baraza hilo, Askofu mkuu Gervas Nyaisonga, lilisema pia maji ya baraka ya kuchovya yatasitishwa kwa muda.

Wakati wa kutakiana amani, TEC imewataka waumini wasipeane mikono na waamini wafumbe mikono na kuinamiana kwa heshima na waamini watakomunika kwenye mikono tu.