Kabudi asema urais ni vipindi viwili tu

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema vipindi viwili vya urais ni kati ya mambo aliyosimamia Mwalimu Julius Nyerere na bado yanaendelea kufanyiwa kazi.

Amesema hayo wakati mjadala wa muda wa urais ukianza kushika kasi baada ya mwananchi mmoja kufungua shauri Mahakama Kuu akiomba tafsiri ya ibara ya 49 (2) inayozuia mtu aliyeshika urais kwa vipindi viwili, kuchaguliwa tena, na hivyo kukivuta chama cha ACT -Wazalendo kuomba kuunganishwa kikisema kina maslahi katika suala hilo.

Pia mwananchi mwingine amewasilisha barua yake Mahakama Kuu akiomba kuunganishwa na muwasilisha maombi wa kwanza.

Jana, Profesa Kabudi alisema Serikali iliyoko madarakani inasimamia Katiba inayosema ukomo wa urais ni wa vipindi viwili pekee na amewataka wananchi wasihusishe jambo hilo na mtu aliyefungua kesi hiyo.

Akizungumza katika kongamano la Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Profesa Kabudi alisema Katiba ndiyo moyo wa Taifa na kwamba, ukomo wa urais umo ndani yake.

Alisema mbali na ukomo huo, suala la Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar litaendelea kuenziwa licha ya changamoto zilizopo.

“Lazima kuendelea kuwa wamoja. Mwalimu Nyerere hakuwa na simile kwa waliojaribu kutikisa Muungano na huu ndio Muungano pekee wa hiari uliobaki duniani licha ya changamoto zilizopo,” alisema Profesa Kabudi.

Waziri huyo alisema ipo misingi iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere ambayo inalitambulisha Taifa.

Aliitaja misingi hiyo kuwa ni uhuru, utu, usawa, haki, kujitegemea, umoja, uadilifu, amani, utaifa, uzalendo na kuwajibikaji.

Akizungumza katika kongamano hilo, mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Udsm, Profesa Rwekaza Mukandala alisema ingawa Mwalimu Nyerere aling’atuka urais Oktoba 1985, alifanikiwa kuzima juhudi za waliotaka kuondoa ukomo wa urais kuwa madarakani.

“Ushawishi wake uliwezesha kukubalika kwa mapendekezo ya Tume ya Bomani kuhusu utaratibu wa kumpata Makamu wa Rais wa Tanzania na mwaka 1995, alitoa mchango mkubwa wa kumpata mgombea urais kupitia CCM,” alisema Mukandala.

“Si tu alihakikisha wagombea wawili waliokuwa wanaongoza wanaachwa, ila alihakikisha mtu wake anapata ushindi kwa hiyo alipoaga dunia kulikuwa na kila sababu ya kuwa na wasiwasi.”

Alisema kutokana na muktadha huo, Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Kigoda cha Mwalimu Nyerere Taaluma za Umajumui wa Afrika, wameandaa kongamano ili kupata fursa ya kutathmini kiwango cha jitihada za kutekeleza malengo makuu ya yaliyosimamiwa na kiongozi huyo.

Akizungumza katika kongamano hilo, spika wa zamani, Anne Makinda alisema Baba wa Taifa alipenda demokrasia na kulikuwa na upinzani licha ya kuwapo chama kimoja.

“Mwalimu alikuwa muumini mkubwa wa demokrasia, aliunga mkono wabunge kusema ukweli,” alisema Makinda.

Alisema muundo wa sasa wa demokrasia haupo sawa kwa sababu wabunge wanapenda zaidi vyama vyao kuliko kusimamia hoja za wananchi.

“Wakati wa mwalimu demokrasia bungeni ilikuwa juu, ilikuwa mtu akishika shilingi kipindi cha mawaziri kusoma bajeti wanapata hadi BP lakini sio sasa,” alisema.