Kafulila awaonya walimu, waratibu elimu Songwe

Muktasari:

Walimu wakuu na waratibu elimu mkoani Songwe nchini Tanzania wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo lasivyo watachukuliwa hatua ikiwamo kupoteza nafasi zao.

Mbozi. Katibu Tawala mkoani Songwe nchini Tanzania, David Kafulila amesema wasimamizi wa elimu na walimu mkoani humo wameshindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo hali inayoufanya mkoa huo kushuka kitaaluma.

Kafulila ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 6, 2019 wakati akifungua kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2020.

Amesema licha ya kushindwa kutimiza majukumu kwa baadhi ya walimu huku wasimamizi wao, waratibu elimu kata na walimu wakuu wakishindwa kuchukua hatua imekuwa sababu kubwa ya kushuka kitaalamu.

Amewaagiza wakuu wa wilaya zote mkoani humo licha ya kusimamia ujenzi wa miundombinu wasimamie utendaji kazi wa walimu na pale inapodhihirika mwalimu mkuu ni mlegevu asiyeweza kusimamia shule au mratibu elimu kata kushindwa kutimiza wajibu wake aondolewe mara moja.

"Tunayo hazina kubwa ya watu wenye sifa ya kuwa walimu wakuu na wanaostahili kuwa waratibu, hivyo wasiyofanya vizuri waondolewe.”

“Kuwaacha kutafanya mkoa kuendelea kushuka kutoka nafasi ya 17 kitaifa mwaka jana na kushika nafasi ya 21 kitaifa mwaka huu,” amesema Kafulila

Kwa upande wake, Ofisa elimu mkoa Songwe, Juma Kaponda amesema wanafunzi 20,345 waliandikishwa kufanya mtihani wa darasa la saba 2019.

Aidha Kaponda kulingana na uchambuzi wa matokeo hayo wasichana wamefaulu kwa asilimia kubwa zaidi ukilinganisha na wavulana.