Kakobe amtaka shahidi video anayohusishwa Askofu Gwajima

Muktasari:

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe amesema ili kanisa liweze kutikisika ni lazima kuwapo na ushahidi wa vinywa ili kuthibitisha kuwa video ile kweli ni ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa na Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema kwa sababu ya uwepo wa picha za video zinazomuonyesha mtu anayefanana na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, lazima kujiuliza kama inawezekana kukubali maudhui yaliyo ndani ya video hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 12 katika mahubiri ndani ya  Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Gwajima.

Amesema wazee wa kanisa watawalao vyema wanastahili kuheshimiwa mara dufu hivyo zinapotokea tuhuma kama za video zilizosambazwa zikimuhusu Askofu Gwajima maandiko yanawaagiza kuwa wasikubali mashtaka juu ya mzee ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.

“Mungu alifahamu uwezekano wa wazee hao kuzushiwa mambo yenye kuchafua huduma na kuwapakaza uchafu na kuharibu kazi hivyo msikubali mashtaka haya hadi vigezo vizingatiwe.”

 “Katika video iliyosambazwa mshtaki yupo wapi kama amejificha na hataki kuonekana. Katika biblia hizo zinaitwa fitina. Mshtaki amejificha polisi ndio wanamsaka, sasa unajificha nini wakati unataka mtu ashughulikiwe kuna nini nyuma,” amesema Kakobe.

Amesema katika video ile mwanamke anayedaiwa kutembea na Gwajima sura yake haionekani hivyo kutokana na suala lile kanisa haliwezi kutikiswa kirahisi.

“Mimi sina mchezo na dhambi, sikuja hapa kutetea uzinzi katika kanisa letu ni wakali sana kuhusiana na masuala ya uzinzi,” amesema Kakobe.