Kala Jeremiah aja na kampeni ya ‘Kijana Smart’

Monday October 21 2019

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Tanzania, Kala  Jeremiah, amekuja na kampeni ya ‘Kijana Smart’ iliyolenga kuamsha ari na hamasa kwa vijana kujitambua ili kuja kupata  jamii itakayoleta matokeo chanya.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 ambapo shirika lake la WanaNdoto ndio itaisimamia.

Jeremiah ambaye ni zao la shindano la Bongo Star Search (BSS), msimu wa kwanza mwaka 2007, amesema amefikia hatua hiyo kama moja ya njia ya kumfumbua na kumuonyesha kijana fursa zinazomzunguka katika maeneo aliyopo ili kujikwamua kiuchumi.

“Tunaamini kijana akijikwamua kiuchumi jamii nzima inakwamuka kwa kuwa kijana ni nguzo muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema

Hata hivyo, amesema kijana hawezi kuwa smart kwa kujikwamua kiuchumi peke yake ila ni rahisi kijana mwenye kipato kumfanya kuwa smart na kushiriki kwenye mambo ya kijamii ndio maana yeye akajitolea kuifanya kazi hiyo kupitia kipato kidogo anachokipata kwenye muziki wake.

Amebainisha kwamba katika kampeni hiyo kipaumbele ni kumuandaa kijana kuwa na utayari wa kutumia vizuri akili na nguvu zake kwa kuzibadili changamoto za jamii yake kuwa fursa kwake na watu wengine  na kuzitambua fursa mbalimbali zinaopatikana katika mazingira aliyopo.

Advertisement

“Ili kijana kufikia huku tumeweka baadhi ya kanuni ikiwemo kuhakikisha anapinga  kwa vitendo mimba  na ndoa za utotoni na kushiriki katika masuala ya jinsia, anakuwa mzalendo na taifa lake, anapambana na maambukizi ya Ukimwi kwa kuwa mwaminifu na kutoa elimu kwa wengine,” amefafanua.

Kampeni hiyo iliyobeba kauli mbiu ya ‘Anza sasa, anza ulipo, anza na ulichonacho’ imelenga pia kubadili fikra za kijana kuwa ili afanikiwe lazma aende eneo jingine  ikiwemo majiji  makubwa katika kutafuta ajira bila kujua hata maneno yao asili wanaweza kuyatumia.

Katika kuwafikia vijana kwenye  kampeni hiyo Jeremiah amesema watakuwa wakifanya kupitia mitandao ya kijamii, nyimbo, Midahalo, kwenda shuleni na kuandaa matamasha.

Advertisement