Kamati mbili zaundwa kuchunguza chanzo moto soko la Tegeta

Muktasari:

  • Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kinondoni imeunda kamati mbili kuchunguza chanzo cha moto ulioteketeza vibanda zaidi ya 80 na maduka 14 katika soko la Tegeta Nyuki, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kinondoni imeunda kamati mbili kuchunguza chanzo cha moto ulioteketeza vibanda zaidi ya 80 na maduka 14 katika soko la Tegeta Nyuki, Dar es Salaam.

Usiku wakuamkia leo Jumatatu Februari 18, 2020 moto ambao chanzo chake hakijajulikana uliteketeza soko hilo la nafaka na matunda na baadhi ya maduka yanayolizunguka.

Akizungumza na Mwananchi leo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel  Chongolo amesema tayari ameunda kamati mbili zitakazochunguza chazo pamoja na madhara ya moto huo.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia madhara yaliyotokea nimeunda kamati mbili, moja kwaajili ya kuchunguza chanzo na nyingine itachunguza hasara,” amesema Chongolo.

Chongolo amesema kamati hizo zitakazofanya kazi kwa siku tatu zitahusisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wataalam wa manispaa ya Kinondoni.

Kuhusu moto huo ulivyoanza, mlinzi wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Abiogwa amesema saa 4.45 usiku moto ulianzia kwenye moja ya duka la mfanyabiashara aliyemtaja kwa jina moja la Bonge na kuanza kusambaa.

Amesema kwa kushirikiana na baadhi ya watu waliokuwa karibu walijaribu kuuzima bila mafanikio na kuamua kupiga simu Zimamoto.

"Tulisikia mshindo wa nguvu ghafla tukaona moto mkubwa unaanza kuwaka kwenye fremu ya Bonge na kuanza kusambaa kwenye soko la matunda na nafaka,” amesema Abiogwa.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Tegeta Pwani,  Evodi Msafiri amesema kati ya fremu 95 zilizozunguka soko hilo 14 zimeteketea na hakuna kitu chochote kilichookolewa.

"Fremu 14 na vizimba 81 vyote vimeteketea na hakuna chochote kilichookolewa hadi sasa chanzo cha moto na hasara havijajulikana,” amesema Msafiri.

Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kinondoni, Peter Mtui amesema moto huo umechelewa kuzimika kutokana na ukubwa wake, walianza kudhibiti ili usisambae kwenye maeneo mengine.