Kamati yataka Bunge likatae kufanya kazi na CAG

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imeliomba Bunge kuridhia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kulidharau na kushusha hashima ya Bunge

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imeliomba Bunge kuridhia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kulidharau na kushusha hashima ya Bunge.

Akisoma ripoti ya kamati hiyo bungeni leo Aprili 2 mwaka 2019 (Jumanne), mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka amesema kamati yake imemtia hatia kwa kuvunja kifungu cha 26 E cha Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Amesema Profesa Assad wakati wa mahojiano na kamati hiyo alionyesha dharau na hakuonyesha kujutia maneno yake.

Amesema  Profesa Assad amesema bila kupima athari yake alizungumza katika redio ya kimataifa na huko ni kukosa uwajibikaji wa pamoja ni tabia mbaya.

“CAG ni mteule wa Rais na kutokana na kuonyesha dharau katika kamati, hakuomba msamaha wala kujutia, Bunge haliko tayari kufanya kazi na CAG na haliko tayari kushirikiana naye kutokana na majukumu yake,”amesema.