Kamati za maadili zazidi kung’ata wagombea

Muktasari:

Zikiwa zimebaki siku 11 kufikia Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 ukiba, kamati za maadili zimeendelea kutoa kuwang’ata wagombea wanaodaiwa kukiuka taratibu.

Dar/Mikoani. Zikiwa zimebaki siku 11 kufikia Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 ukiba, kamati za maadili zimeendelea kutoa kuwang’ata wagombea wanaodaiwa kukiuka taratibu.

Adhabu ambazo zimekwishatolewa hadi sasa ni pamoja na kuzuiwa kufanya kampeni kuanzia siku tano hadi wiki mbili na mmoja ametakiwa kuomba radhi kupitia vyombo vya habari kwa siku saba.

Wakati hadi sasa ni wagombea kutoka vyama kadhaa vya upinzani waliokumbanana adhabu hizo, Katibu wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Taifa ameeleza kuwapo malalamiko yaliyowasilishwa dhidi ya CCM ambayo yameshughulikiwa.

Baadhi ya wanasiasa waliokwisha kumbanana na adhabu za kamati hiyo ni Tundu Lissu ambaye amemaliza kutumikia adhabu ya kutofanya kampeni kwa siku saba kwa madai ya kukiuka maadili baada ya kulalamikiwa na vyama vya CCM na NRA.

Aidha, juzi Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilimtia hatiani mgombea urais kupitia ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad (pichani) na kumpa adhabu ya kumfungia siku tano akidaiwakwenda kinyume na maadili ya uchaguzi.

Kama ilivyokuwa kwa Lissu, Maalim Seif ambaye ni mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, alisema hatakata rufaa akidai kuwa hana imani na ZEC.

“Kwanza sitokataa rufaa, pili ni jambo nililolitarajia, hivyo sikushtuka hata kidogo. Naamini CCM ina hofu ya mkutano wangu wa Nungwi,” alisema Maalim Seif.

Adhabu kwa wagombea ubunge

Ukiondoa wagombea urais kupewa adhabu ya kuzua kampeni, mgombea ubunge wa jimbo la Serengeti kwa tiketi ya Chadema, Catherine Ruge jana alijikuta akipewa adhabu ya kutakiwa kuomba radhi kwa siku saba mfululizo kupitia vyombo vya habari na katika mikutano ya hadhara.

Pia ametakiwa kumuomba radhi kwa maandishi msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ikiwa ni utekelezaji wa kipengele cha 5.11(a) cha maadili ambacho kinaagiza upande uliokiuka maadili kusahihisha kosa au makosa yaliyotendeka.

Mbali na Ruge, mgombea udiwani kata ya Nyansurura katika jimbo hilo, Francis Garatwa naye wa Chadema amesimamishwa kufanya kampeni kwa muda uliobaki sambamba na kuondolewa kwenye timu ya kampeni ya mbunge.

Pia Garatwa ametakiwa kulipa faini ya Sh700,000 na kuomba radhi kwa umma kupitia vyombo vya habari akidaiwa kukiuka maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2020.

Msimamizi wa jimbo la uchaguzi la Serengeti, Juma Hamsini alisema “kamati ya maadili iliyoketi Oktoba 15 ikishirikisha wajumbe kutoka Chadema ilifikia uamuzi huo dhidi ya Garatwa ambaye ni Mwenyekiti wa chama wilaya ya Serengeti kwa kosa la kuvamia ofisi ya msimamizi na kufanya fujo.”

Katibu wa Chadema wilaya hiyo, Julius Antony alithibitisha kushiriki kikao na kupokea barua akisema wanakusudia kukata rufaa.

Ruge na Garatwa walikamatwa Oktoba 12 kwa tuhuma za kuvamia ofisi ya msimamizi wa jimbo na kusababisha uharibifu wa vifaa wakishinikiza kupewa ratiba mpya ya kampeni.

Hata hivyo, Ruge aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kuwa hataomba radhi kama alivyotakiwa na kamati hiyo.

“Jana (juzi) nimeletewa barua hii baada ya kamati ya maadili kukaa, wamenihukumu bila hata kuniandikia tuhuma zangu wala kuniita kujitetea kwenye kamati.

@TumeUchaguziTZ fundisheni wasimamizi wenu kufuata kanuni za uchaguzi na maadili ya uchaguzi. #SitaombaRadhi,” aliandika.

Ruge na Garatwa wameingia katika orodha ya wabunge na madiwani walioonja joto ya kamati hizo, wakiwamo Halima Mdee (Kawe) aliyezuiwa kufanya kampeni kwa siku saba tangu Oktoba 12 hadi Oktoba 18.

Mgombea mwingine wa Chadema aliyekumbwa na adhabu hiyo ni mgombea ubunge wa Ubungo, Boniface Jacob aliyezuiwa kwa siku saba, huku Gervas Mgonja wa Same Magharibi naye akitakiwa kutofanya kampeni kwa siku 14.

Adhabu kama hizo pia zimewakumba pia Aisha Luja (Manyoni Mashariki) wa Chadema na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kutoka CUF aliyesimamishwa kwa siku 10.

Katika Jimbo hilo madiwani wa kata 18 wa CUF pia walisimamishwa kufanya kampeni kwa siku 10

Kamati ya Taifa yafafanua

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Katibu wa kamati ya maadili ya uchaguzi ya Taifa, Emmanuel Kawishe alikanusha dhana kwamba malalamiko yanayotolewa na kuamuliwa ni ya upande wa upinzani pakee.

Alisema Kamati inapokea malalamiko ya na inayafanyia kazi.

‘‘Mwenendo wa uchaguzi unakwenda vizuri, vyama vinazingatia maadili wanapoonywa wanazingatia. Niseme tu wagombea wanazingatia maadili na sheria za nchi.

“Hao wanaosema malalamiko hayajatangazwa, mbona kuna wengine wameletewa malalamiko na yameshughulikiwa? Ukiona imetangazwa maana yake ni mojawapo ya adhabu za kifungu cha 5.11,” alisema Kawishe.

Kifungu hicho kinataja moja ya adhabu ni kumtangaza mgombea au chama kinacholalamikiwa kwenye vyombo vya habari.

“Malalamiko mengine yanaletwa na vyama vinaitwa, wajumbe wakikutana wanafanya uamuzi, anayeonekana kutokuwa na hatia anakuwa hana hatia,” alisema.

Hivi karibuni, mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alidai kuwa chama hicho kimepeleka malalamiko matatu katika kamati hiyo lakini hayajatangazwa na hakuna dalili ya kushughulikiwa.

Akijibu madai hayo, Kawishe alisema: “Moja wapo ya adhabu za maadili ni kukitangaza chama au mgombea kwenye vyombo vya habari (kuwa amelalamikiwa), kwa hiyo hilo swali halijibiki. Kwa sababu nikikwambia wagombea hawa wameadhibiwa maana yake mimi nitakuwa nimewaadhibu.”

Alipoulizwa kuhusu hatua ya Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk Wilson Mahera kumtangaza Lissu kuwa amekiuka maadili kabla kamati ya maadili haijamsikiliza, Kawishe alisema kilichofanywa ni utekelezaji wa kifungu cha 4.1(g) kinachoeleza maadili kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kifungu hicho kinasema, “Kukemea vitendo vyenye nia ya kuharibu uchaguzi vinavyoweza kufanywa na viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao, Serikali au vyombo vyake.”

Imeandikwa na Elias Msuya, Bakari Kiango na Anthony Mayunga.