Kamishna TRA ataja mambo mawili yanayowakwamisha wahitimu nchini

Friday November 22 2019

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dk Edwin Mhede amesema baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na tamaa, kutumia maarifa vibaya.

Amesema wanapewa maarifa kwa ajili ya kuyatumia kujiingizia kipato lakini baadhi wanayatumia kupata utajiri wa haraka na kujiingiza katika vitendo vya rushwa.

Dk Mhede ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 22, 2019 katika mahafali ya 12 ya Chuo cha Kodi.  Wanafunzi 424 wamehitimu katika ngazi mbalimbali.

“Leo mmehitimu mtambue kazi ni ibada lakini pia kazi ni amri hivyo katumieni maarifa yenu kwa ajili ya kujiingizia kipato.”

“Mkibahatika kuajiriwa msiendekeze usingizi Taifa linawategemea katika ukusanyaji wa kodi lakini pia kuelimisha jamii kuhusu ulipaji kodi,” amesema.

Ameongeza  TRA itaendelea kuunga mkono jitihada za chuo hicho kuhakikisha kinatoa elimu bora ya ukusanyaji wa kodi.

Advertisement

Sultan Emmanuel, mhitimu katika ngazi ya stashahada amesema atajikita zaidi kuelimisha Watanzania umuhimu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Advertisement